Kwa ufupi, mijadala ya  Mkutano wa Nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi COP30 inazunguka maswali makubwa matatu:

1) Nchi zinawezaje kuongeza kasi ya kuchukua hatua za kukabili mabadiliko ya tabianchi?

Pamoja na ongezeko la joto duniani kwa kasi na majanga ya hali ya tabianchi yakizidi kuwa makali, kupunguza hewa ukaa na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na athari zake kunachukua nafasi ya juu kwenye ajenda. Wajumbe wanaangazia zana muhimu kama vile:
Mchango ya Kitaifa (NDCs): Mipango ya kitaifa ya hali ya hewa inayohuishwa kila baada ya miaka mitano. Katika COP30, nchi zinajadili njia mpya za kuongeza azma na kasi ya utekelezaji.
Kuondokana na nishati ya kisukuku: COP28 ilikubaliana “kuhama kutoka kwa mafuta ya kisukuku.” Sasa, wajumbe wanajadili kuweka ramani wazi zaidi ya mabadiliko hayo kulingana na muktadha wa kila nchi.
Mipango ya Kitaifa ya Uhimilivu au Mnepo (NAPs): Nchi 72 zimewasilisha mipango yao, lakini nyingi hazina ufadhili. Mapendekezo mojawapo: mara tatu ya fedha za uhimilivu ifikapo 2025.
Lengo la Kimataifa la Uhimilivu au Mnepo: Mazungumzo yanahusu takribani viashiria 100 vya kufuatilia maendeleo ya uhimilivu duniani.
Mpango Ufadhili wa Misitu: Tayari inaungwa mkono na nchi 36 zinazowakilisha asilimia 45 ya maeneo ya misitu duniani na asilimia 65 ya Pato la Dunia. Lengo ni kufidia pengo la dola bilioni 66.8 kwa mwaka kwa ajili ya kulinda na kurejesha misitu ya tropiki.

2) Fedha na teknolojia zinawezaje kuwafikia wanaohitaji zaidi?

Ahadi za kisiasa pekee haziwezi kutatua mzozo wa tabianchi zinahitaji rasilimali halisi. Wajumbe wa COP30 wanatafuta njia za kufungua ufadhili na teknolojia:
Kifungu cha 9.1 cha Mkataba wa Paris: Nchi zilizoendelea lazima zisaidie kifedha nchi zinazoendelea. Wajumbe wanatafakari mpango kazi na njia za uwajibikaji.
Ramani ya Baku–Belém ya Dola Trilioni 1.3: Pendekezo la kutoa dola trilioni 1.3 kwa mwaka kwa nchi zinazoendelea, likiwa na maeneo matano ya hatua na nyenzo zisizoongeza mzigo wa madeni.
Mfuko wa Hasara na Uharibifu: Ulioundwa katika COP27 na kuzinduliwa COP28 ili kusaidia nchi zilizoathirika vibaya na athari za tabianchi. Unawasili COP30 ukiwa na upungufu mkubwa wa fedha, na hivyo kuibua wito wa michango zaidi.
Mfuko wa Tabianchi Kijani: Mfuko mkubwa zaidi wa hali ya hewa duniani, lakini duru yake ya hivi karibuni ya uchangishaji imeonyesha kupungua.
Mfuko wa Mazingira Ulimwenguni (GEF): Hutolewa kwa nchi zinazoendelea, lakini kiwango cha sasa kinachukuliwa kuwa hakitoshi.
Mpango wa Utekelezaji wa Teknolojia: Unalenga kuongeza upatikanaji wa teknolojia za tabianchi, lakini mazungumzo yamekwama kuhusu vikwazo vya fedha na biashara.
Hatua za kibiashara zinazozuia upatikanaji wa bidhaa: Sera za biashara zinazohusiana na hali ya hewa zinazoathiri zaidi nchi zinazoendelea. Wazo moja: kuunda jukwaa la kutathmini athari zake.

3) Hatua za tabianchi zinawezaje kuwa za haki na jumuishi?
Hata kukiwa na ufadhili, mabadiliko makubwa yanaweza kuongeza ukosefu wa usawa ikiwa hayatalinda jamii zilizo hatarini. Wajumbe wanatengeneza mifumo ya kuhakikisha usawa na ujumuishi:
Mpango wa Mabadiliko ya Haki (Just Transition): Unalenga haki ya kijamii, ajira bora, na maendeleo endelevu. Nchi zinatarajia mfumo wa vitendo unaolingana na hali halisi ya wafanyakazi na jamii.
Mpango wa Hatua za Kijinsia: Unaongoza ujumuishaji wa usawa wa kijinsia katika hatua za hali ya hewa. Mpango wa kwanza ulipitishwa 2017; toleo lililoboreshwa linatarajiwa kupitishwa COP30.

Kwa nini uamuzi wa Belém ni muhimu

Uamuzi utakaofanywa Belém utaamua jinsi Mkataba wa Paris utatekelezwa kwa vitendo, na kama malengo ya dunia ya tabianchi yanaweza kufikiwa. Ndani ya vyumba vya mazungumzo, ujumbe ni mmoja: muda haupo, na maelewano hayawezi kusubiri. Uamuzi huu utaamua sio tu kasi ya kupunguza hewa ukaa, bali pia kama haki itatendeka kwa watu wa asili, pamoja na Afrika na nchi zinazoendelea ambazo zinabeba mzigo mkubwa wa athari za tabianchi licha ya kuchangia kidogo kwenye tatizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *