
Vikosi va Msaada wa Haraka nchini Sudan (RSF) na Falme za Kiarabu, nchi inayodaiwa kuwaunga mkono, siku ya Ijumaa, Novemba 21, wamekaribisha nia ya Donald Trump ya kukomesha vita vya mauaji ya kuwania madaraka vinavyoiangamiza Sudan. Juhudi hizi za kidiplomasia zinakuja huku nchi hiyo ikiwa eneo la “mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu” duniani, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Imechapishwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Mnamo Novemba 19, rais wa Marekani alisema kwamba alitaka kukomesha “ukatili” nchini Sudan baada ya Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman kumtaka aingilie kati ili kukomsha vita, ambavyo vimewaua maelfu na kusababisha mamilioni ya watu kutoroka makazi yao tangu mwezi Aprili 2023.
Kufuatia hili, Baraza Kuu la Sudan, linaloongozwa na mkuu wa jeshi, Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan, pia limebainisha utayari wake wa kushirikiana na Washington na Riyadh kujaribu kukomesha mzozo huo.
Mnamo Novemba 21, Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), vinavyoendelea na vita dhidi ya jeshi, vilisema kwamba vilikuwa vinatoa “majibu kamili na mazito kwa mipango hii” huku pia vikikosoa uongozi wa jeshi la Sudan. “Tunathibitisha (…) kwamba kikwazo halisi cha kufikia amani ni kundi linalodhibiti maamuzi ya vikosi vya jeshi, linaloundwa na mabaki ya utawala wa zamani na viongozi wa kundi la kigaidi la Muslim Brotherhood,” RSF ilitangaza katika taarifa iliyotolewa kwenye Telegram.
Mkuu wa vikosi vya kijeshi, Jenerali Mohamed Daglo, mara kwa mara huwasilisha mzozo huo kama mapigano dhidi ya “Waislamu wenye msimamo mkali” upande wa upinzani, ingawa yeye mwenyewe alishirikiana na Jenerali al-Burhan mnamo mwaka 2021 kuwaondoa raia madarakani.
Falme za Kiarabu zakaribisha juhudi za Trump
Falme za Kiarabu, nchi ambayo mara kwa mara inashutumiwa kuunga mkono wanamgambo wa RSF inayopigana dhidi ya jeshi la Sudan, pia zimekaribisha siku ya Ijumaa kujitolea kwa Rais wa Marekani Donald Trump kukomesha vita nchini Sudan. Wakati wa mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Falme za Kiarabu Abdullah bin Zayed Al Nahyan “amekaribisha kauli za Rais wa Marekani Donald Trump akitaka kukomeshwa kwa mashambulizi ya kutisha yanayofanywa dhidi ya raia” na kusifu jukumu lake “kama kiongozi katika kuanzisha utulivu nchini Sudan,” UAE, mwanachama wa juhudi za upatanishi, imesema.
Mnamo Septemba, kundi la upatanishi linalojulikana kama “Quad,” ambalo pia linajumuisha Marekani, Misri, na Saudi Arabia, lilipendekeza mpango unaotaka kusitishwa kwa mapigano kwa miezi mitatu na kutengwa kwa serikali ya sasa na vikosi vya RSF katika mazingira ya kisiasa baada ya migogoro—kifungu ambacho hadi sasa kimekataliwa na jeshi huku mazungumzo yakikwama.
Mwanzoni mwa mwezi Novemba, RSF walitangaza kwamba wamekubali kusitishwa kwa mapigano baada ya kuchukuwa udhibiti wa El-Fasher, ngome ya mwisho ya jeshi katika jimbo la Darfur (magharibi), ambapo Umoja wa Mataifa umeripoti mauaji ya halaiki, ubakaji, uporaji, na kusababisha watu wengi kutoroka makazi yao.
Sasa wakiwa wanadhibiti Darfur, eneo kubwa nchini Sudan na linalojumuisha theluthi moja ya eneo la ardhi la Sudan, RSF wameongeza mashambulizi yao katika wiki za hivi karibuni katika jimbo jirani la Kordofan, eneo lenye utajiri wa mafuta. Kwa siku kadhaa, wamekuwa wakitangaza “ukombozi unaokaribia” wa mji wa Babanousa, ambao wamekuwa wakiuzingira tangu mwezi Januari 2024. Babanousa ni mojawapo ya miji ya mwisho huko Kordofan Magharibi inayoshikiliwa na jeshi na kituo cha reli cha kimkakati kinachounganisha magharibi mwa nchi na Khartoum.
EU yamwadhibu naibu mkuu wa RSF
Huko Brussels, kufuatia mkutano wa Mawaziri 27 wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, vikwazo viliwekwa dhidi ya naibu mkuu wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) nchini Sudan. Hii inamhusu Abdelrahim Daglo, kaka wa kiongozi wa RSF Mohamed Hamdane Daglo, anayejulikana pia kama Hemedti, ambaye anatuhumiwa kwa ukatili dhidi ya raia. Vikwazo hivyo ni pamoja na marufuku ya kuingia EU na kuzuiwa kwa mali zake: “Hii inatuma ishara kwamba jumuiya ya kimataifa itawashtaki wale waliohusika,” imesema Brussels.
Kwa raia wa Sudan, waathiriwa wa vurugu kali za vita hivi, uamuzi wa kuwawekea vikwazo naibu kiongozi wa RSF unaonekana kutokuwa na madhara ikiwa wahusika wengine wa uhalifu huu, na kiongozi wao Mohamed Hamdane Daglo, pia hawatawekewa vikwazo.