Msemaji wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa, amevikosoa vyombo vya habari vya kimataifa kwa kile amesema hivi karibuni vimetoa ripoti za upande mmoja kuhusu vurugu zilizoshuhudiwa wakati na baada ya uchaguzi wa Octoba 29.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Msigwa alivitaja vyombo vya habari kama BBC, CNN, Aljazeera na DW kuwa miongoni mwa vyombo vilivyoripoti kile amekisema habari ambazo hazikuzingatia weledi.

Msigwa ametolea mfano makala ya hivi karibuni iliyotolewa na shirika la habari la Marekani CNN, makala ambayo imeibua mjadala mkali nchini humo.

Katika makala hiyo ambayo iliandaliwa na mwanahabari raia wa Kenya, Larry Madowo, ilitumia teknolojia za kisasa kubaini maeneo na umbali waliokuwa askari wakati wakiwafyatulia risasi waandamanaji kwenye miji ya Arusha na Dar es Salaam.

Aidha kwenye makala hiyo, CNN ilionesha kile imedai bado haijathibitisha sehemu ambayo huenda waliouawa wakati wa uchaguzi walizikwa kwa pamoja.

Kama ambavyo chombo hiki kimefanya katika ripoti zake mbalimbali, kimeendelea kufanya makosa yakiuweledi na kiuadilifu katika uandishi wa habari, kwa kutangaza na kuchapisha maudhui ambayo yanaegemea upande mmoja. Sio kweli, kwamba CNN ilishindwa kupata upande wa Serikali. Alisema Msigwa

Inashangaza kuona chombo cha habari cha kimataifa kama CNN kufanya makosa makubwa ya kimaadili kama haya ambayo yamefanywa.

Msigwa pia aliitaka CNN kuwasiliana na Serikali kwa lengo la kuchapisha maudhui ya kweli, akihoji kwanini hakikuzingatia kanuni ya haki hata kwa anayetuhumiwa.

Kuhusu idadi ya watu waliouawa wakati wa maandamano ya Octoba 29, Msigwa amesema tathmini bado inaendelea na kwamba idara ya polisi ndio yenye mamlaka ya kutangaza ni watu wangaoi walipoteza maisha, huku akisisitiza kuwa kazi moja wapo ya tume iliyoundwa hivi karibuni ni pamoja na hilo.

Kuhusu uvumi wa maandamano ya Desemba 9, Msigwa aliwaonya vijana wa Tanzania akiwataka kutojihusisha na vitendo vyovyote vya vurugu au kushawishiwa kufanya vurugu kwa lengo la kuharibu amani ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *