
Wakfu wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki umekosoa vikali zoezi la uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Tanzania Oktoba 29, 2025.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kulingana na Wakfu huo, Tanzania kwa sasa haina serikali halali, ukisisitiza kuwa mazungumzo ya kweli na yanayojumuisha pande zote ndio njia pekee inayoweza kuliepusha taifa hilo kutumbukia katika mzozo wa kisiasa.
Katika taarifa iliyochapishwa Novemba 23, 2025, Wakfu huo ulieleza kuwa, matokeo ya uchaguzi wa wabunge na urais yaliotangazwa na Tume huru ya uchaguzi nchini humo, INEC hayakuwa ya kweli na hayakuonyesha mapenzi ya Watanzania.
Ripoti ya Wakfu huo imeonekana kukubaliana na walichosema baadhi ya waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa wakiwemo wale wa kutoka (SADC) na (AU) ambao wote walisema uchaguzi huo haukufikia vigezo vya kimataifa vinavyostahili kuufanya uwe uchaguzi halali na haki.
Licha ya kwamba Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameonyesha kuwa tayari kwa mazungumzo ya maridhiano pamoja na kuzindua Tume ya kuchunguza kilichotokea wakati wa uchaguzi huo, upinzani umetupilia mbali.
Chama kikuu cha upinzani CHADEMA kilikosoa tume iliyoundwa na Rais kuchunguza kilichotokea, kikisema hakina imani na tume za ndani.
Chadema kinataka taasisi za kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa, Mahakama ya ICC pamoja na SADC kupewa majukumu ya kufanya uchunguzi.
Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa Volker Türk, Novemba 11, 2025, alitoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi kamili kubaini chanzo za mauaji yaliotokea wakati wa uchaguzi wa urais nchini Tanzania.