Katibu Mkuu anawakumbuka wale wote ambao wameathirika au kupoteza maisha kutokana na mashambulizi ya kemikali kwa miaka mingi, akizitaja mbinu hizo kuwa “za kuchukiza” na kinyume na misingi ya sheria za kimataifa.

Maadhimisho ya mwaka huu yana umuhimu wa kipekee kwani yanatimiza miaka 100 tangu kukubaliwa kwa Itifaki ya Geneva ya mwaka 1925, mkataba muhimu uliounganisha mataifa baada ya kutikiswa na madhara ya hofu ya silaha za kemikali katika Vita vya Kwanza vya Dunia kupiga marufuku matumizi yake katika vita.

Guterres amebainisha kuwa juhudi za kimataifa tangu wakati huo zimeleta maendeleo makubwa, ikiwemo kupitishwa na karibu ushiriki wa ulimwengu mzima katika Mkataba wa Silaha za Kemikali, unaokataza utengenezaji, uzalishaji, uwekaji akiba na matumizi ya silaha hizo.

Hata hivyo, anaonya kuwa tishio bado lipo. “Matumizi ya kutisha ya silaha za kemikali yameendelea,” anasema, akiongeza kuwa kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia inaweza kufanya iwe rahisi zaidi kutengeneza na kutumia silaha hizo.

Katibu Mkuu anatoa wito kwa mataifa yote kuthibitisha upya dhamira yao ya dunia isiyo na silaha za kemikali, akiongeza kusema, “kwa niaba ya waathiriwa wote wa vita vya kemikali, nahimiza nchi kuthibitisha upya kujitolea kwao kwa dunia isiyo na silaha hizi za kuchukiza.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *