MSHAMBULIAJI wa Namungo, Fabrice Ngoy amesema kitu pekee kinachombeba kwa sasa ni kutokana na ushirikiano wa wachezaji wenzake na kuaminiwa na benchi la ufundi, jambo linalomuongezea motisha ya kupambana kila anapopata nafasi ya kucheza.
Kauli ya nyota huyo inajiri baada ya juzi kuifungia Namungo bao moja katika ushindi wa timu hiyo wa 1-0, dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, ambapo kwa sasa amefikisha mabao matatu ya Ligi Kuu tangu msimu huu umeanza.
“Sijiangalii peke yangu kwa sababu naamini katika ushirikiano na wenzangu, hata bao nililofunga kama nisingepewa pasi nisingefanya kile nilichokifanya, kitu kikubwa ninachopambana ni kutengeneza uaminifu kwa benchi la ufundi,” amesema.
Aidha, Ngoy amesema baada ya kufikisha mabao matatu na kuivunja rekodi yake binafsi ya msimu uliopita alipofunga mawili, kwa sasa anataka ahakikishe anafunga zaidi ili kuipambania timu hiyo, kutokana na ushirikiano mzuri anaoupata kwa nyota wenzake.
Nyota huyo ameaminiwa na kocha, Juma Mgunda, licha ya uwepo wa washambuliaji wengine wakiongozwa na Mkongomani mwenzake, Heritier Makambo aliyetoka TRA United zamani Tabora United na Abdulaziz Shahame ‘Haaland’, aliyetokea kikosi cha TMA.
Ngoy alijiunga na Namungo msimu wa 2023-2024, akitoka Kitayosce iliyobadilishwa jina na kuitwa Tabora United na sasa TRA United, baada ya kuifungia mabao 15 ikiwa Ligi ya Championship, nyuma ya kinara, Edward Songo wa JKT Tanzania aliyefunga 18.
Mshambuliaji huyo alitua nchini kwa mara ya kwanza 2022-23, akitokea Real Nakonde FC ya Zambia, na msimu uliopita akiwa na Namungo alifunga mabao 2.