Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) imefungua njia kwa wanariadha wa Urusi na Belarus kushiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya 2026 baada ya kubatilisha marufuku iliyowekwa na Shirikisho la Kimataifa la Michezo ya Ski na Snowboard (FIS). CAS imesema wanariadha wanaokidhi vigezo vya IOC vya kushindana kama washindani huru wanapaswa kuruhusiwa kushiriki katika mashindano ya kufuzu.
Urusi imepokea uamuzi huo kwa furaha, ikisema ni ushindi mwingine baada ya mahakama kadhaa kutoa maamuzi yanayowarusu wanariadha wake wa michezo mingine kama bobsleigh na luge kushiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Milan-Cortina. Waziri wa michezo wa Urusi ameutaja uamuzi huo kama ushindi wa tatu mfululizo kwa Urusi katika michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi.
FIS ilitangaza mnamo Oktoba kuwa ilikuwa imepiga marufuku wanariadha kutoka Urusi na Belarus kushiriki katika mashindano ya kufuzu, hatua iliyofuata baada ya kuzuiliwa kwao tangu 2022 kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Hata hivyo, wanariadha hao walikuwa wakitarajia kushindana chini ya bendera huru bila kuwakilisha mataifa yao.
Mnamo Septemba, IOC ilitangaza kuwa wanariadha wa Urusi na Belarus wanaweza kushiriki Olimpiki chini ya bendera zisizo za kitaifa ikiwa watatimiza masharti maalum, ikiwamo kutoshiriki katika timu, kutokua na uhusiano na jeshI, na kutokuwa na msimamo wa kuunga mkono vita. Masharti haya yalitumika pia katika Olimpiki za Paris 2024, ambako wanariadha kutoka mataifa hayo walishinda jumla ya medali tano.
Njia kwa wanariadha wa Urusi, Belarus kushiriki paralimpiki
Marufuku ya FIS ilikuwa pigo kwa wanariadha wa ski wa Urusi ambao waliibuka na mafanikio makubwa katika Olimpiki za Beijing 2022 kwa kushinda karibu theluthi moja ya medali za mchezo huo. Hata hivyo, CAS ilikubali rufaa za mashirikisho ya ski ya Urusi na Belarus, ikisema kanuni za FIS zinakataza ubaguzi na zinakilazimisha chombo hicho kuwa huru kisiasa.
Uamuzi wa CAS pia unafungua njia kwa wanariadha wa Urusi na Belarus kufuzu kwa Michezo ya Paralimpiki. Kamati ya Paralimpiki (IPC) iliondoa baadhi ya vikwazo kwa wanariadha hao, lakini ilisema ni wachache sana wanaoweza kufuzu. Hadi sasa, Urusi imekuwa ikikabiliwa na marufuku ya bendera yake kwenye mashindano ya kimataifa tangu 2016 kutokana na kashfa ya matumizi ya dawa za kutunisa misuli na baadaye uvamizi wa Ukraine.
Belarus nayo ilikumbwa na adhabu mwaka 2022 kwa kuruhusu ardhi yake kutumika kuisaidia Urusi kuvamia Ukraine. Tangu wakati huo, mataifa yote mawili yamezuiwa kushiriki mashindano mengi ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na soka. Hata hivyo, baadhi ya mashirikisho ya michezo yameanza kulegeza masharti, yakiruhusu wanariadha wa mataifa hayo kurejea hatua kwa hatua.
Hivi karibuni, Shirikisho la Judo la Urusi lilisifu “uamuzi wa kihistoria” wa shirikisho la kimataifa la mchezo huo (IJF) kuruhusu wanajudo wa Urusi kushindana chini ya bendera yao ya taifa. Uamuzi huo umepokelewa kwa ukosoaji mkali na Shirikisho la Judo la Ukraine, likiutaja kama kinyume cha amani, haki na uwajibikaji.
Chanzo. AFPE