
Kocha Mbelgiji wa Cameroon Marc Brys siku ya Jumatatu alifutwa kazi, na golikipa wa Manchester United Andre Onana hakujumuishwa kwenye kikosi cha Afcon 2025 inayotarajiwa kuanza Disemba 21 nchini Morocco.
Brys amekuwa na uhusiano mbaya na rais wa shirikisho la soka la taifa hilo na mchezaji nyota wa zamani Samuel Eto’o kwa hiyo kutimuliwa kwake siyo jambo la ajabu baada ya timu hiyo kushindwa kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026.
Cameroon, ambayo imecheza katika ngazi ya Kombe la Dunia mara nane na ni rekodi kwa bara la Afrika, ilifungwa na timu ambayo haikupewa nafasi ya Cabo Verde ili kupata nafasi ya moja kwa moja kuelekea kwenye michuano hiyo itakayofanyika Marekani, Canada na Mexico.
Wakapata fursa ya pili kama moja ya timu nne bora zilizomaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi, Cameroon ikafungwa 1-0 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo nchini Morocco mwezi uliopita na kuondolewa.