Wengi wanadai kuwa Rais Donald Trump aliyeongoza zoezi la kusaini mkataba huo ana maslahi ya kiuchumi kwa Marekani na si amani ya mashariki mwa Kongo.
Ni mkataba ambao ulisubiriwa kwa muda mrefu na kwa hamu kama tumaini la kipekee la kuvimaliza vita vya miaka thelathini sasa mashariki mwa Kongo Marais wa Rwanda Paul Kagame na Felix Tshisisekedi wa Kongo wakatia saini mkataba wa kuzika tofauti zao.
Rwanda wahoji M23 kutengwa
Hata hivyo baada ya kusainiwa mkataba huo wananchi wa Rwanda wanahisi nguvu za kusitisha mapigano na kuleta usalama mashariki mwa Kongo zinaelekezwa upande usiotakiwa kwa kuwa wanaopigana ni serikali ya Kongo na waasi wa AFC/M23 na si Kongo na Rwanda.
Jean Batiste Gasominari ambaye ni mwanasheria kitaaluma na mchambuzi wa siasa za maziwa makuu anasema kusainiwa kwa mkataba ni vizuri lakini kamwe hakuwezi kuleta suluhu
“Unajua kusaini mkataba ni kitu kimoja na kutekeleza ni kitu kingine… Nataka tutofautishe vitu viwili vinavyoendelea, hayo yanayotokea ni kati ya Kongo na waasi wa M23 na si kati ya Kongo na Rwanda,” alisema.
Wakati haya yakiendelea, mapigano makali yanaendelea mashariki mwa Kongo hasa kuelekea katika mji wa Uvira unaopakana kwa ukaribu sana na nchi ya Burundi.
M23 wazidi kujiimarisha kivita
Ijumaa, baadhi ya waandishi wa habari upande wa Rwanda wanaoishi katika mpaka wa Rwanda na Burundi lakini karibu na Kongo wamesema kuna hali ya utulivu wakati M23 wakiendelea kuimarisha mikakati yake kwa kuongeza idadi ya wapiganaji kuanzia usiku wa kuamkia Ijumaa.
Jean Uwera ni mwandishi wa habari wa muda mrefu na mchambuzi wa siasa za Maziwa Makuu anasema kwa kuwa M23 haijapewa kipaumbele ni wazi kwamba mapigano hayo hayatasimama.
Amesema “Mapigano hayawezi kusimama kwa sababu M23 haiko Washington ni lazima Kinshasa iwe mwaminifu,Trump yeye anazingatia mambo ya kiuchumi.”
Mkataba huu baina ya Rwanda na Kongo unazitaka nchi mbili kusitisha uhasama mara moja kupitia kusitisha mapigano, lakini pia kuanzisha mchakato wa ushirikiano wa kiuchumi katika masuala ya madini yanayopatikana mashariki mwa Kongo.
