Mkakati huu mpya unaitaka Marekani kutazama upya na kufanya marekebisho katika sera yake ya kigeni hasa kuhusu uwakilishi wake wa kijeshi katika maeneo mbalimbali ya ulimwengu, kuhamisha rasilimali zake kutoka kwenye matumizi ya mbali na kwenda katika kukabiliana na masuala kama uhamiaji dawa za kulevya na usalama wa kikanda.
Akizungumza kuhusu mkakati na sera hiyo Rais Donald Trump kwa mara nyingine ametetea sera yake ya Marekani kwanza akisema mkakati huo unakwenda sambamba na kuitekeleza sera hiyo.
Hata hivyo sehemu ambayo imewafanya baadhi ya wadadisi kujiuliza maswali mengi katika mkakati huo ni matumizi ya lugha kali zinazotumiwa kwa washirika wa Marekani wa Ulaya. Mkakati huo unaonya Umoja wa Ulaya kwa kusema unakabiliwa na kupoteza maadii pamoja na kuzorota kiuchumi, tatizo la uhamiaji, mabadiliko ya idadi ya watu na kupotea kwa umaarufu na ushawishi wa bara la Ulaya.
Ripoti kuhusu sera na mkakati huu wa Marekani kwa mataifa ya kigeni imetishia kwamba bara la Ulaya huenda litakuwa halitambuliwi tena ndani ya kipindi cha miaka 20 kuanzia sasa ikiwa hali ya sasa haitarekebishwa.
Marekani kuunga mkono mrengo wa kulia Ulaya?
Katika hali isiyotegemewa sera hii imesisitiza kwamba Marekani itakwenda mbali kupinga mustakabali wa sasa wa siasa za Ulaya hali ambayo inatishia kwamba sasa Marekani inaweza kuunga mkono vyama vya mrengo mkali barani Ulaya vyenye sera sawa na Marekani kuhusu suala la uhamiaji, uzalendo na utaifa.
Hata hivyo Ujerumani imejibu madai kuhusu sera hii mpya ya Marekani na mkakati wake, waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani Johann Wadephul amesema Marekani haina mamlaka ya kutoa ushauri kuhusu mwelekeo wa ulaya na Ujerumani.
“Marekani itaendelea kuwa mshirika wetu muhimu katika mfungamano wetu, hata hivyo muungano wetu kazi yake ni kukabiliana na changamoto za kiulinzi na kiusalama, na bila shaka ni muungano wenye tunu zake lakini tunasema matatizo mengine yanaweza kujadiliwa pembeni, naendelea kuamini kuwa suala la uhuru wa kutoa maoni na kujitawala ni maswala ya ndani ya Ujerumani.”
Mataifa ya Ulaya yamshangaa Trump
Mkakati huu wa Marekani kuhusu sera yake nje umezikasirisha nchi za Umoja wa Ulaya huku nyingi zikishangazwa na azma ya Rais Trump kuhusu kuyaunga mkono makundi na vyama vinavyolenga kuvunja au kudhoofisha uwepo wa Umoja wa Ulaya. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani Johann Wadephul amesema wao kama nchi hawahitaji ushauri kutoka nje kwa sababu wana uwezo kujitatulia mambo yao wenyewe.
Amesema “Shirikisho la Ujerumani hadi sasa limeweza kujadili masuala haya yote ya ndani kwa ufasaha na mafanikio makubwa. Na sisi tunajiona kama watu wenye kuweza kujadili mambo hata katika siku za usoni sisi wenyewe na kwa hili hatuhitaji msaada kutoka nje.”
Sehemu ya mkakati huu wa Marekani inaeleza wazi kwamba Rais Trump anataka kuachana na fikra na sera za kuwa kiongozi wa dunia huku lakini akiendelea kuwa makini na kuimarisha juhudi za kuzuia ushawishi wa China ambayo sasa ni mshindani mkuu wa Marekani wa kiuchumi kuliko kijeshi.