Serikali imewataka wananchi wabaki majumbani mwao kwa ajili ya sherehe za Uhuru wa taifa hilo la Afrika Mashariki.

Wanaharakati wameitisha maandamano kupinga ushindi wa chama tawala cha CCM katika uchaguzi wenye utata uliofanyika Oktoba 29, ambao ulisababisha siku kadhaa za maandamano ambapo mamia ya watu waliuawa na zaidi ya watu 2,000 walikamatwa.

Ukaguzi na upekuzi jijini Dar es Salaam

Maandamano hayo yalidumu kwa siku tatu huku waandamanaji wakichoma magari, vituo vya kupigia kura na vituo vya mafuta wakitaka matokeo yaliyomtangaza Rais Samia Suluhu Hassan kushinda kwa zaidi ya asilimia 97 yafutwe.

Magari ya polisi na askari kwa miguu walipiga doria Jumanne Asubuhi katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam, makao makuu ya utawala Dodoma na jiji la kaskazini mashariki la Arusha, huku vizuizi vya barabarani vikiwekwa karibu na maeneo muhimu ya serikali ikiwemo Ikulu na ulinzi mkali jijini Dar es Salaam na Dodoma

Adha ya usafiri wa umma

Hakukuwa na usafiri wa umma jijini Dar es Salaam Jumanne baada ya wamiliki wa mabasi kuondoa magari yao, wakihofia kurudiwa kwa uharibifu wa mali uliotokea Oktoba. Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba Jumatatu aliwataka wafanyakazi wasio wa lazima wabaki nyumbani Jumanne.

Hali ya utulivu katika maeneo ya barabara kuu ya Dar es Salaam.
Hali ya utulivu katika maeneo ya baadhi ya barabara kuu za Dar es Salaam.Picha: Eric Boniface/DW

Sherehe za kila mwaka za Uhuru zilifutwa mwezi Novemba na serikali ikasema fedha ambazo zingetumika kwa sherehe hizo zitatumika kukarabati miundombinu iliyoharibiwa. Vyama viwili vikuu vya upinzani nchini vilizuiwa kutopeleka mgombea kukabiliana na Rais Samia, ambaye ni makamu wa rais wa zamani aliyepandishwa cheo kufuatia kifo cha mtangulizi wake, John Pombe Magufuli.

Kiongozi mkuu wa upinzani, Tundu Lissu, alitaka mageuzi ya uchaguzi kabla ya kura za Oktoba yupo kizuizini tangu Aprili akikabiliwa na mashtaka ya uhaini. Shirika la utetezi wa haki za binaadamu la Human Rights Watch mapema Jumatatu lilikemea ukandamizaji dhidi ya wanaharakati wa Tanzania, likisema angalau watu 10 wamekamatwa tangu katikati ya Novemba kufuatia machapisho ya mitandao ya kijamii kuhusu maandamano yaliyopangwa.

Amnesty: Tanzania iheshimu haki ya kukusanyika kwa amani

Kadhalika Amnesty International pia ilitoa taarifa Jumatatu ikihimizaTanzania kuheshimu haki ya kukusanyika kwa amani na ikionya dhidi ya kuzimwa kwa mtandao tena kama ilivyokuwa kwa zaidi ya wiki moja baada ya uchaguzi wa Oktoba.

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Ijumaa iliitaka serikali ya Tanzania “kuepuka kutumia nguvu kuvunja mikusanyiko isiyo na vurugu na kufanya kila jitihada kupunguza mvutano.”

Makundi kadhaa ya wanaharakati wa Kenya yalionyesha mshikamano na wenzao wa Tanzania na kuisihi serikali ichunguze mauaji na watu waliopotea wakati wa maandamano ya Oktoba. Hata hivyo serikali ya Tanzania imeunda tume ya kuchunguza vurugu za baada ya uchaguzi lakini matokeo yake bado hayajatangazwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *