
Rais wa Afrika Kusini alisema Jumatatu kuwa “chochote kilicho chini ya uhuru wa Palestina na kutambuliwa kwa haki za msingi za binadamu za watu wa Palestina hakitakubalika na hakitapelekea amani ya haki na endelevu katika eneo hilo.”
Akiwahutubia wajumbe wa Baraza Kuu la Kitaifa la Tano la Chama cha African National Congress (ANC), Cyril Ramaphosa alisema nchi yake ina wasiwasi kuwa Israel inaendelea kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano na kundi la kupigania ukombozi wa Palestina la Hamas ambayo yalianza kutekelezwa Oktoba 10.
Ramaphosa aliwaambia wajumbe wa chama huko Ekurhuleni karibu na Johannesburg kuwa: “Afrika Kusini ilikaribisha makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yalileta kurudi kwa mateka na kuachiliwa kwa wafungwa wengi wa kisiasa wa Palestina. Hata hivyo, kuna jambo la wasiwasi zaidi kwamba Israel inakiuka makubaliano ya kusitisha mapigano karibu kila siku.”
Alisema uhalifu uliotekelezwa na Israel dhidi ya watu wa Gaza ulifanya serikali yake kupeleka kesi mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ikieleza kuwa utawala wa Israel unakiuka majukumu yake chini ya Mkataba wa Kuzuia Uhalifu wa Kimbari.
Afrika Kusini ilipeleka kesi dhidi ya Israel kwenye ICJ mwezi Desemba 2023, kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza na kuuawa kwa raia. Tangu wakati huo, mahakama imetoa hatua za muda za kuagiza Israel kuchukua hatua za kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari.
Ramaphosa alisema: “Tangu mashambulizi ya Israel yaanze Oktoba 7, 2023, zaidi ya watu 70,000 wameuliwa kuuliwa Gaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.”
Kwingineko katika hotuba yake, Rais wa Afrika Kusini amesema: “Lazima pia tuwe na wasiwasi kuhusu mateso makubwa yanayosababishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe Sudan, ambako inaripotiwa kuwa zaidi ya watu 150,000 wameuawa.”