Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na za pamoja za kukomesha mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Amir Saeid Iravani alitoa matamshi hayo jana Jumanne katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ulioadhimisha miaka 10 ya Siku ya Kimataifa ya Kukumbuka Waathiriwa wa Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari.

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba ukimya hauwezi kufuta uhalifu wala mateso ya waathiriwa wake, akisisitiza kwamba kukabiliana na mauaji ya kimbari si jambo la hiari, bali ni wajibu wa kisheria na kimaadili.

“Tunasisitiza azma yetu kubwa ya kupambana na kuzuia uhalifu wa mauaji ya kimbari,” amesema Iravani akisisitiza kwamba dunia inapaswa kuchukua hatua “kwa azma, kwa pamoja na mara moja” ili kukomesha ukatili huo na kulinda heshima ya wale walioathiriwa.

Iravani ameeleza kuwa Jamhuri ya Kiislamu, kama mfadhili mwenza wa azimio lililoanzisha Siku ya Kimataifa ya Kukumbuka Waathiriwa wa Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari, inawakumbuka waathiriwa wote ambao mateso yao “yanailazimisha jamii ya kimataifa kutenda kwa uhakika na uwazi wa kimaadili.”

Amesisitiza kwamba kuzuia mauaji ya kimbari ni wajibu unaotokana na sheria za kimataifa na jukumu la mataifa yote.

Balozi wa Iran UN amesisitiza kwa kusema: “Ni wajibu wetu wa pamoja kuzuia na kuwaadhibu wahusika wa mauaji ya kimbari popote na wakati wowote tishio la mauaji ya kimbari linapotokea.” 

Utawala wa Kizayuni wa Israel ulianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza Oktoba 2023 na hadi sasa umeua Wapalestina zaidi ya 70,400, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *