Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) amesema kwamba “kinachoendelea huko Gaza hakijawahi kushuhudiwa tangu wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.”

Adnan Abu Hasna ameitaja hali ya sasa katika Ukanda wa Gaza kuwa isiyo ya kawaida na kusema: “Sehemu kubwa ya eneo hilo haiwezi tena kuwa makazi ya watu kutokana na uharibifu na kuzingirwa; na utawala wa Kizayuni ndio wa kulaumiwa kutokana na hali hiyo.”

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amefichua kwamba: “Mamia ya maelfu ya mahema na malori 6,000 yaliyobeba misaada ya kibinadamu yanasubiri kuingia Gaza, lakini utawala vamizi wa Israel unayazuia.”

Abu Hasna ameendelea kusema: “Hali ya binadamu katika Ukanda wa Gaza imeripotiwa kuwa mbaya sana kutokana na vikwazo vikali vinavyozuia kuingizwa misaada katika eneo hilo la Palestina.”

Hapo awali, msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) alikuwa amesema kwamba misaada inayowasili katika Ukanda wa Gaza haikidhi mahitaji ya chini kabisa ya wakazi wa eneo hili.

Hazem Qassem amesema: “Malori mengi yaliyoingia Ukanda wa Gaza yalikuwa yamebeba bidhaa za biashara na za sekta binafsi, na vilevile bidhaa ambazo, licha ya janga la binadamu, zinatambuliwa kuwa zisizo za dharura kwa wakazi wa Ukanda wa Gaza.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *