Dar es Salaam. Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeingia tena katika taswira mpya ya machafuko, ikiwa ni mfululizo wa miaka mingi ya ghasia ambazo zimelifanya eneo hilo kuwa kitovu cha vita visivyokoma.

Mashambulizi ya waasi wa M23 yameibuka tena yakishika kasi katika hali inayovuruga makubaliano ya amani yaliyofanyika wiki iliyopita yakipewa matumaini makubwa kuwezesha kusitisha mzozo huo. Zaidi ya watu 25,000 wamekimbia mkazi yao tangu kuanza upya kwa mzozo huo mapema mwezi huu.

Wiki iliyopita, Desemba 4, 2025, viongozi wa DRC na Rwanda walikutana Washington D.C. Marekani na kusaini ‘Makubaliano ya Washington,’ Marekani akiwa msimamizi wa mchakato wa kurejesha amani katika ukanda huo wa Maziwa Makuu.

Hivyo, kuzuka upya kwa mapigano siku chache baada ya kusaini makubaliano hayo kunaonesha ukosefu wa uaminifu baina ya pande husika na udhaifu wa mkataba wenyewe katika utelekezwaji wa mikakati iliyosainiwa kwa makubaliano ya pande zote mbili ambayo inaonekana kukosa nguvu ya kudumu.

Mazungumzo hayo yaliyoongozwa na Rais wa Marekani, Donald Trump na kuhudhuriwa na Marais Felix  Tshisekedi wa Congo DRC, Paul Kagame wa Rwanda na William Ruto wa Kenya yamefanyika kipindi ambacho kwa wiki kadhaa, Vikosi vya M23 vimeripotiwa kupanua maeneo yake, vikichukua miji muhimu ya mashariki mwa Congo.

Hatua hiyo imeuibua Umoja wa Afrika (AU) ambao kupitia kamisheni yake, umelaani kuendelea kwa mapigano hayo loicha ya juhudi zinazochuliwa katika kuhakikisha mzozo huo unakomeshwa na kutoa fursa kwa wananchi kuendelea na maisha yao bila bughuza.

Kupitia taarifa iliyotolewa jana Desemba 11, 2025, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Mahmoud Ali Youssouf, amelaani kuendelea kwa mashambulizi ya M23 Mashariki mwa Congo akitoa wito wa kusitishwa kwake mara moja. 

“Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, anafuatilia kwa wasiwasi mkubwa hali inayoendelea katika eneo la Maziwa Makuu, hususan matukio ya Kivu Kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na pia katika Jimbo la Cibitoke, Burundi,” imesema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mapigano yanayoendelea yanaweza kuathiri ukanda mzima wa maziwa makuu zikiwemo nchi za Congo yenyewe, Rwanda, Burundi na mataifa mengine jirani.

“Mwenyekiti anaonyesha kuguswa na idadi ya raia walioathirika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi, anasisitiza kuhusu msimamo wa muda mrefu wa Umoja wa Afrika kwamba amani ya kudumu katika eneo la Maziwa Makuu inategemea heshima kamili ya mamlaka na uadilifu wa  Mataifa yote,” imesema taarifa hiyo.

Aidha, mbali na kulaani mashambulizi hayo AU pia imetoa wito kwa Mataifa yote katika ukanda wa Maziwa Makuu kuheshimu wajibu wao chini ya Mkataba  wa Addis Ababa na kuzingatia kikamilifu  msingi wa kutoshambuliana na Kulindana wa Mkutano wa Kimataifa wa Eneo la Maziwa Makuu.

Mizizi ya Mapigano na juhudi za amani.

Mgogoro mashariki mwa Congo una historia ndefu, ukianzia katika migogoro ndani ya Taifa hilo mwanzoni mwa miaka ya 2000 na kuendelea kwa makundi mengi ya waasi yanayoshindania udhibiti wa maeneo mbalimbali katika Taifa hilo kubwa zaidi la Ukanda wa Maziwa Makuu.

Aidha, utajiri mkubwa wa madini kama dhahabu na cobalt, pamoja na misuguano ya kikabila imekuwa ikitajwa kama chanzo cha migogoro ambayo imekuwa ikilikumba Taifa hilo, hadi mwaka 2012, ambapo kundi la M23 liliibuka rasmi likidai kutetea haki za jamii.

Kwa zaidi ya miongo miwili, maeneo ya Kivu yamekosa utulivu, na kila jaribio la amani limekwama katika mtego wa maslahi ya kisiasa na kiuchumi huku M23 limekuwa likihusishwa na ushirikiano wa mataifa jirani na udhibiti wa rasilimali za Taifala Congo DRC, hali iliyofanya mashariki mwa Congo kuwa mojawapo ya maeneo yenye mgogoro ya muda mrefu zaidi duniani.

Kwa kipindi chote hicho, raia wa maeneo hayo wameendelea kuishi kwa madhila ya vita, mauaji, ubakaji, njaa,  kuporomoka kwa uchumi na kukimbia makazi wakivuka mipaka kuelekea Burundi, Rwanda na Uganda, hali inayotishia utulivu wa eneo lote la Maziwa Makuu.

Katika juhudi za kusitisha mapigano na kurejesha amani, juhudi za kikanda na kimataifa zimekuwa zikichukuliwa mara kadhaa bila mafanikio. Mojawapo ya juhudi hizo ni zile za kikanda ndani ya Afrika zikihusisha Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Jumuiya hizi zimekuwa zikifanya mazungumzo ya  mara kwa mara, ikiwemo kupeleka vikosi maalum vya kijeshi kusaidia kurejesha utulivu, lakini utekelezaji wake umekumbwa na changamoto nyingi, ikiwemo ukosefu wa rasilimali na maelewano finyu ya kisiasa.

Katika juhudi za Kimataifa, mapema mwaka huu 2025, Qatar iliandaa majadiliano yaliyolenga kuweka msingi wa usitishaji mapigano kati ya DRC, Rwanda na wadau wengine. Makubaliano hayo ya hatua za mwanzo yalipokelewa kwa matumaini makubwa, yakirejea dhamira ya pande husika kuweka mazingira ya kupunguza mapigano na kuruhusu misaada ya kibinadamu.

Taarifa ya Doha ilisema pande zote zimekubali kuheshimu makubaliano ya kusitisha vita na kuruhusu utekelezaji wake, hata  hivyo, ndani ya wiki chache tu, mapigano yaliibuka tena katika maeneo ya Kivu Kaskazini, yakionesha wazi udhaifu wa utekelezaji wa makubaliano hayo.

Katika hatua za hivi karibuni, Mnamo Desemba 4, 2025, viongozi wa DRC na Rwanda walikutana Washington D.C. Marekani na kusaini ‘Makubaliano ya Washington D.C,’ ambayo Marekani imekuwa msimamizi wa mchakato wa kurejesha amani katika ukanda huo wa Maziwa Makuu, ambapo Marais wa Congo na Rwanda waliahidi kumaliza mgogoro huo.

“Makubaliano haya ya Washington lazima yawe ishara ya kujitoa kwetu bila kurudi nyuma katika kutafuta amani ya kudumu kwa watu wetu,” alisema Rais Tshisekedi akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo nchini Marekani.

Kwa upande wake, Rais  Kagame alipozungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, alieleza kuwa makubaliano hayo ni mwisho wa mgogoro uliodumu kwa muda mrefu katika eneo hilo akisema linahitajika suluhisho la kudumu baada ya miaka mingi  ya mvutano.

Ingawa matamshi hayo yalionesha matumaini, mapigano mapya yaliyozuka siku chache baada ya kusaini makubaliano hayo, M23 kuendelea kufanya mashambulizi, kunaonesha wasiwasi ikiwa makubaliano hayo yana nguvu ya kudumu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *