KIUNGO mshambuliaji wa Stand United ya Shinyanga, Raymond Masota amelibebesha mzigo Shirikisho la Soka nchini (TFF) kukomalia programu za kuandaa wachezaji chipukizi (TDS) ili kusaidia kutibu changamoto ya muda mrefu ya Tanzania kukosa washambuliaji wenye sifa.

Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikikabiliwa na tatizo la washambuliaji matata wenye uwezo mkubwa wa kutumia nafasi, ambapo mara nyingi Timu ya Taifa (Taifa Stars) imekuwa ikilazimika kutumia mawinga na viungo washambuliaji kupata mabao.

Vilevile, timu nyingi za Tanzania zikiwamo Simba na Yanga zimekuwa zikilazimika kwenda nje ya nchi kusaka washambuliaji wakali watakaotikisa nyavu za wapinzani, huku washambuliaji wachache wazawa waliopo wakikosa mwendelezo.

Masota anayemudu kucheza nafasi ya beki wa kulia, wingi zote na kiungo mkabaji, aliliambia Mwanaspoti kuwa vituo vya TFF Mnyanjani Tanga, Karume na Kigamboni, vitaleta matunda siku za usoni na kutibu tatizo hilo.

“Nadhani mabadiliko yanachukua muda mrefu sana, binafsi nina imani kubwa sana na chama cha mpira (TFF), mwanzo haikuwa hata rahisi kufuzu mashindano kama CHAN (Kombe la Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani) na AFCON (Kombe la Mataifa ya Afrika),” amesema.

Aliongeza; “Tuwape muda waendelee na mchakato tunawaona vijana wanaotengenezwa na vituo kama TDS naamini ipo siku tutafika tunapopataka.”

Masota ambaye amekaa nje ya uwanja kwa mwaka mmoja tangu Desemba 21, 2023 akiuguza jeraha la goti, msimu huu amerejea kwenye soka akijiunga na Stand United ya Shinyanga inayoshiriki Ligi ya Championship, ambako tayari ameshafunga bao moja na kutoa asisti mbili.

Pia aliwahi kucheza Ken Gold FC na Geita Gold msimu wa mwaka 2023/2024 ikiwa Ligi Kuu Bara na kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *