STRAIKA wa Simba aliyesimamishwa mechi tano kwa kosa la utovu wa nidhamu, Jonathan Sowah amevunja ukimya na kusema licha ya kupewa adhabu hiyo na Bodi ya Ligi, lakini ukweli tukio alilolifanya kwa Himid Mao wa Azam FC halikuwa la kukusudia kumpiga kiwiko bali alikuwa akiwania mpira.

Nyota huyo aliyetua Msimbazi akitokea Singida Black Stars akiwa ameifungua jumla ya mabao 14 kupitia mechi 15, yakiwamo 13 ya Ligi Kuu kupitia mechi 14 na moja la nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) amefungiwa mechi tano na fainali ya Sh1 milioni kwa kumpiga kiwiko Himid katika mechi ya Mzizima Derby ambapo Simba ililala kwa mabao 2-0.

Akizungumza na Mwanaspoti, Sowah amesema kama mchezaji anasikitika kwa adhabu aliyopewa, lakini ukweli ni kwamba hakudhimiria kumpiga Himid ila alikuwa akiwania mpira na kwa bahati mbaya mkono wake ukamgusa kiungo huyo mkongwe.

Sowah amesema kama mchezaji aliyekuwa akiipambania timu iliyokuwa nyuma kwa mabao 2-0 alitaka kuzuia shambulizi kwa wakati huo na alifanya hivyo kwa sababu Azam ilikuwa inaongoza mchezo huku Simba ikiwa inapambania kujikomboa.

“Wakati Himid ameanguka nilidhani kama anajifanyisha ndio maana nilikuwa namwambia ainuke tuendelee na mechi, sikujua kama nimemgonga, (alipolala chini) nikahisi ni katika ya mbinu za kimchezo hasa wapinzani wanapokutangulia wanaanza kupoteza muda,” amesema Sowah na kuongeza;

“Mimi si mchezaji mkorofi, naomba hilo niliweke wazi maana naona kuna kampeni inaendelea chini kwa chini kurudisha nyuma kazi yangu.”

Straika huyo aliongeza kwa kusema amekuwa akisikia na kuona anajadiliwa kama mtovu wa nidhamu, lakini anajua siku zote mti wenye matunda ndio unaopigwa mawe.

“Hili nimeliona muda mrefu kwani msimu uliopita niliingia dirisha dogo na nilifunga mabao mengi, lakini hawakuniweka hata kwenye orodha ya tuzo ni kama hakuna nilichofanya,” amesema Sowah na kuongeza;

“Halafu msimu ndio kwanza unaanza na mimi nakosa mechi tano muhimu kwangu hili ni zaidi ya adhabu, najihisi vibaya kukaa nje, huku mashabiki wangu wakinikosa uwanjani ila naamini haya yatapita tu.”

Kabla ya kutua Singida BS katika dirisha dogo, Sowah alitokea Al Nasr ya Libya, alikoondoka akiwa amecheza nusu msimu na kufunga mabao saba.

Hata alivyotua Singida mashine hiyo ilionyesha kiwango bora, huku akiifungia timu hiyo mabao 13 ndani ya nusu msimu, akibakiza hatua chache kumfikia Jean Ahoua aliyekuwa akiongoza ligi akiwa nayo 16.

Sowah atakosa mechi tano kwa mujibu wa ratiba ambapo Simba itacheza dhidi ya Mtibwa Sugar, Singida Black Stars, KMC, TRA United na Tanzania Prisons.

Hata hivyo, mwishoni mwa msimu uliopita katika mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga, Sowah alilimwa kadi nyekundu iliyomfanya akose pambano la Ngao ya Jamii la ufunguzi wa msimu huu na mechi moja ya Ligi Kuu 2025-26 dhidi ya Fountain Gate.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *