Ile michuano maarufu zaidi ya Kombe la Mapinduzi inaanza leo Visiwani Zanzibar huku mwaka huu ikitegemewa kuwa na msisimko mkubwa zaidi.

Michuano hiyo inayofahamika kama Kombe la Mapinduzi 2026 inaanza kwa kupigwa mechi mbili za Kundi A mchezo wa kwanza ukiwa ni ule wa watetezi Mlandege dhidi ya Singida Black Stars ambao utapigwa saa 10:15 jioni kabla ya saa 2:30 usiku Azam FC itakwaruzana na URA ya Uganda.

Huu ni msimu wa 20 tangu michuano hiyo ilipoanza kwa mfumo wa sasa mwaka 2007, huku kwa miaka 18 imeshuhudiwa mechi zinazohusisha klabu mbalimbali kabla ya mwaka huu (2025) kutumiwa na timu za taifa zilizokuwa zikijiandaa na michuano ya CHAN 2024 iliyoandaliwa kati ya Tanzania, Kenya na Uganda na kushuhudiwa wenyeji Zanzibar Heroes ikibeba taji mbele ya Burkina Faso.

Katika michuano ya msimu huu kuna jumla ya timu 10 zikiwamo tano za Tanzania Bara, Simba, Yanga, Azam FC, Singida Black Stars na TRA United pamoja na URA kutoka Uganda na klabu nne za Zanzibar, watetezi wa taji, Mlandege, Fufuni, KVZ na Muembe Makumbi.

Kwa namna waandaaji wa Kombe la Mapinduzi 2026 walivyopanga ratiba ya ufunguzi wa mashindano hayo, ni wazi waliangalia mambo mawili.

Kwanza ushindani ndani ya uwanja, pili burudani kwa mashabiki watakaofika Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja.

Ushindani huo wa ndani ya uwanja na burudani jukwaani kwa mashabiki unatokana na mechi ya kwanza itakayochezwa leo Jumapili Desemba 28, 2025, kisha ile ya pili saa 2:15 usiku zote zikipigwa uwanjani hapo.

Mabingwa mara mbili mfululizo mwaka 2023 na 2024, Mlandege kutoka Unguja, itaikaribisha Singida Black Stars ambayo baada ya Miguel Gamondi kuwa na majukumu ya kuiongoza Taifa Stars katika AFCON 2025, mzigo ameachiwa David Ouma.

Singida Black Stars inashiriki Kombe la Mapinduzi kwa mara ya kwanza, lakini Mlandege inakumbuka wakati inabeba ubingwa wa kwanza na wa pili katika michuano hii, ilizichapa timu za Tanzania Bara.

Mwaka 2023 ilianza kuifunga mabao 2-1 Singida Big Stars ambayo sasa inaitwa Fountain Gate, kisha 2024 ikawa zamu ya Simba kupigwa bao 1-0.

Singida Black Stars ambayo awali ilikuwa ikiitwa Ihefu, ushiriki wao wa mara ya kwanza katika michuano hii hauwezi kubezwa kwani imekuwa ikifanya vizuri ndani na kimataifa katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Ikiwa hatua ya makundi Kombe la Shirikisho ikianza kwa kufungwa, kisha sare, Singida Black Stars inajivunia taji la Kagame ililobeba Septemba mwaka juu jijini Dar es Salaam.

Kwa Mlandege, ukiachana na kutoanza vizuri Ligi Kuu Zanzibar msimu huu ikiwa bingwa mtetezi, lakini imepania kutetea tena Kombe la Mapinduzi ambalo sasa linachezwa kwa kushirikisha timu za klabu baada ya 2025 kuwa timu za taifa.

Kocha Msaidizi wa Mlandege, Sabri China, alisema: “Kama kawaida yetu tumejipanga kufanya vizuri, tunataka kuona ule ubingwa tuliouchukua mwaka 2023 na 2024, tunauchukua tena safari hii ili kuzidi kuonyesha  ubora wetu.”

Kwa upande wa Ouma, alisema: “Hakuna mashindano tunayoshiriki hatuyapi kipaumbele. Kwetu ni fursa nzuri kuwa sehemu ya timu zitakazoshiriki Mapinduzi yatakayokuwa na timu ny[1]ingi shindani. Yatatusaidia kuiweka timu kwenye nafasi nzuri.”

Azam VS URA

Mabingwa wa kihistoria katika michuano hii, Azam itapapatuana na URA kutoka Uganda kuanzia saa 2:15 usiku.

Hii ni mechi ya mabingwa kwani timu zote zimelichukua Kombe la Mapinduzi kwa nyakati tofauti.

Azam ikiwa ndiyo imelibeba mara nyingi zaidi tangu mwaka 2007 ambazo ni tano, imelichukua 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019.

URA imelichukua mara moja pekee mwaka 2016.

Mbali na hilo, hii mechi itaturudisha nyuma hadi 2018, wakati Azam ikitwaa ubingwa wa nne, fainali iliichapa URA kwa penalti 4-3 baada ya dakika tisini ngoma kumalizika 0-0.

Kocha wa Azam, Florent Ibenge alisema: “Azam ni timu kubwa, hakuna shindano tunakwenda bila malengo ya kuchukua ubingwa, ni kweli nataka kila mchezaji kuwa tayari, kama hukupata nafasi kwenye ligi na mechi za CAF, hii ni sehemu ya kuonyesha uwe[1]zo wako kama mchezaji.

“Kama ninavyosema kila wakati nina wachezaji wazuri sana hapa, muhimu ni kila mtu kushindana ili kupata nafasi, tunataka kila mchezaji awe na akili ya namna hiyo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *