Kwa mujibu wa taarifa ya OCHA iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis na Kyiv, raia kadhaa wameripotiwa kujeruhiwa katika mashambulizi hayo yaliyodumu kwa zaidi ya saa 10.

Wakati ving’ora vya tahadhari ya mashambulizi ya anga vilipolia usiku kucha, wakazi walilazimika kujificha kwenye makazi ya dharura, vituo vya treni za chini ya ardhi na maeneo salama zaidi ndani ya nyumba zao huku milipuko ikiripotiwa katika maeneo mbalimbali ya jiji.

media:entermedia_image:481d7e1d-4bfb-4526-8bb8-45d2c029afa3

Mgao wa kuni unaendelea kusaidia watu kukabiliana na msimu wa baridi kali na ukosefu wa umeme Borodianka, katika mji mkuu Kyiv nchini Ukraine

Uharibifu Mkubwa wa miundombinu

Mashambulizi hayo pia yameharibu miundombinu muhimu, na kuwaacha watu wengi bila Vipasha joto wala umeme katikati ya hali ya baridi kali.

OCHA imesema wahudumu wa misaada wanashirikiana na wahudumu wa huduma ya kwanza wa dharura na timu za ukarabati mjini Kyiv, huku ikibainisha kuwa mashambulizi yanaendelea kupanuka na kufikia maeneo yaliyo mbali na mstari wa mapigano.

“Kadiri mashambulizi yanavyopanuka, ndivyo watu walio hatarini zaidi wanavyoathirika zaidi,” shirika hilo limeonya, likieleza wasiwasi mkubwa kwa wazee, watoto na watu wenye ulemavu ambao wako katika hatari kubwa wakati wa kukatika kwa umeme kwa muda mrefu katika majira ya baridi.

Hali inaendelea kuwa tete

Kwa mujibu wa OCHA mashambulizi ya hivi karibuni yameongeza mzigo kwa mfumo wa nishati wa Ukraine ambao tayari uko katika hali dhaifu kutokana na kushambuliwa mara kwa mara tangu kuanza kwa mzozo.

Huku nyumba na shule zikiathirika, mashirika ya kibinadamu yanashirikiana na mamlaka za ndani kutathmini mahitaji na kutoa msaada wa dharura, ikiwemo msaada wa joto, makazi na huduma za msingi.

media:entermedia_image:166f00be-a791-4274-b7b5-ed252948c0d9

Time ya IAEA ikizuru kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhya nchini Ukraine

Juhudi za usalama wa nyuklia zinaendelea

Wakati huo huo, juhudi zinaendelea za kuimarisha upatikanaji wa umeme karibu na Kituo cha Nyuklia cha Zaporizhzhya (ZNPP), kituo kikubwa zaidi cha nyuklia barani Ulaya.

Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) limethibitisha kuwa ukarabati muhimu wa njia za umeme umeanza kufuatia kusitishwa kwa mapigano kwa muda katika eneo hilo, makubaliano yaliyosimamiwa na shirika hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi, amesema timu ya IAEA inafuatilia kwa karibu kazi za ukarabati ambazo zinatarajiwa kuchukua siku kadhaa. Amewashukuru pande zote kwa kukubali “kusitisha mapigano kwa muda ili kuruhusu kurejeshwa kwa usafirishaji wa umeme kati ya vituo vya kubadilishia umeme vya ZNPP na Kituo cha Umeme cha Joto cha Zaporizhzhya, hatua itakayosaidia kuimarisha usalama wa nyuklia.”

Bwana. Grossi amesisitiza kuwa kurejeshwa kwa umeme wa nje kwa uhakika ni muhimu ili kuzuia ajali ya nyuklia wakati wa mzozo wa kijeshi unaoendelea.

Kadiri mapigano yanavyoendelea, mashirika ya Umoja wa Mataifa yameendelea kuonya kuwa mashambulizi yanayoendelea dhidi ya miji na miundombinu muhimu yanaongeza mahitaji ya kibinadamu kote Ukraine, hasa katika miezi migumu ya majira ya baridi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *