Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, leo Desemba 31, 2025, amepiga marufuku vitendo vya uchomaji wa matairi wakati wa kusherehekea mkesha wa Mwaka Mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Tanga, Dkt. Batilda amesema kuwa uchomaji wa matairi ni hatari kwa usalama wa wananchi pamoja na kusababisha uharibifu wa miundombinu, jambo ambalo halikubaliki katika sherehe za kuukaribisha mwaka mpya.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wakazi wa Mkoa wa Tanga kujumuika kwa pamoja katika Uwanja wa Uhuru Park, ambapo sherehe za kuupokea Mwaka Mpya zinafanyika rasmi ngazi ya mkoa, badala ya kusherehekea kwa njia zinazoweza kuhatarisha usalama.

Dkt. Batilda Burian amesema kuwa katika mkesha wa Mwaka Mpya kutakuwepo na mashindano mbalimbali ya mapishi, pamoja na upigaji wa baruti ambao umeandaliwa kwa utaratibu maalumu na salama, ili kuhakikisha sherehe zinafanyika kwa amani na usalama kwa kila mwananchi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Batilda amewashukuru wakazi wa Mkoa wa Tanga kwa kuendelea kudumisha amani na utulivu wakati wote, akisisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi na vyombo vya usalama ndio msingi wa maendeleo na ustawi wa Mkoa huo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *