Wachambuzi wa Kizayuni wamekiri kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel hauna uwezo wa kukabiliana na makundi mapya ya Muqawama wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Moshe Elad, mtaalamu wa kizayuni wa masuala ya usalama amesema, “leo hii mapambano katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan yanapanuka kwa kasi, na tunakabiliana na nguvu na uwezo ambao hatujawahi kukabiliana nao hapo kabla”. Mtaalamu huyo wa kizayuni wa masuala ya usalama ameongezea kwa kusema: “tunashuhudia kupata nguvu makundi yanayojitegemea katika Ukingo wa Magharibi ambayo hayana uhusiano wowote wa kimuundo na kitaasisi na Hamas, Fat-h au Jihadul-Islami, na wakati huo huo, yanapanua wigo wa hatua na harakati zao katika eneo hili”.

Chaneli ya 14 ya televisheni ya utawala wa kizayuni, nayo 14 pia imetangaza katika ripoti yake kwamba, kwa kuendelea usitishaji vita, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina, HAMAS inapanua hatua kwa hatua mamlaka yake ya utawala katika eneo la Ghaza. Luteni Kanali Hezi Nichama, mkuu wa klabu ya makamanda wa akiba wa jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel naye pia ametoa indhari kwa taasisi husika za uchukuaji maamuzi kwamba, utawala huo ghasibu haujafanikiwa kuhitimisha kikamilifu vita vya Ghaza. Chaneli ya 14 ya Israel imeongezea kwa kusema: “kwa ungamo la afisa huyu wa jeshi, ni wazi kwamba tulishindwa kufikia lengo kuu la vita, ambalo ni kuiangamiza Hamas”.

Uungaji mkono wa Wapalestina kwa HAMAS Ghazza

Kuungama huko kwa makamanda na wataalamu wa masuala ya usalama wa utawala wa Kizayuni kunaonyesha kuwa, lengo kuu la vita vya Ghaza ambalo ni kuangamizwa Hamas halijaweza kufikiwa. Kushindwa kufikia lengo hilo kunaonyesha kuwa, katika hali yoyote ile na pamoja na kuungwa mkono kwa hali na mali na Marekani na Magharibi, utawala wa Kizayuni hauna uwezo wa kuuangamiza kikamilifu Muqawama wa Palestina.

Upande mwingine wa ungamo hilo la wataalamu wa kijeshi wa Kizayuni ambao ni kuhusu nguvu na kukubaliwa na umma makundi ya Muqawama ya Palestina unathibitisha jinsi makundi hayo yalivyokita mizizi ndani ya umma wa Wapalestina. Licha ya mashinikizo ya kijeshi na kuwekewa mzingiro, Hamas imeweza pia kudumisha mamlaka yake ya utawala katika Ukanda wa Ghaza.

Lakini mbali na Ghaza, katika Ukingo wa Magharibi pia, sasa yameibuka makundi ya Muqawama yanayojitegemea, ambayo hayana mfungamano na mavuguvugu ya jadi ya Muqawama wa Palestina, yaani Hamas, Fat-h na Jihadul-Islami, jambo linalodhihirisha namna mapambano ya Wapalestina yalivyokita mizizi ndani ya jamii ya Wapalestina wenyewe na yanavyoibuka bila kuhitaji msukumo wa nje.

Wataalamu wa Kizayuni wamekiri kuwa makundi hayo mapya yamepanua wigo wa harakati zao bila ya kuwa na utegemezi kwa harakati nyingine. Hali hiyo ya kujitegemea ya makundi hayo mapya ya Muqawama wa Palestina imetoa changamoto kali kwa utawala wa Kizayuni, kwa sababu hauwezi tena kudhibiti mapambano ya Wapalestina kwa kuyawekea mashinikizo yale makundi maarufu tu na yanayojulikana.

Wanamuqawama wa Palestina

Mapambano ya umma katika Ukingo wa Magharibi nayo pia yamegeuka kuwa vuguvugu pana la kijamii. Mwenendo huo umeuweka utawala wa Kizayuni kwenye makabiliano na wimbi la maandamano ya upinzani na operesheni zisizoweza kutabirika.

Wataalamu na makamanda wa kizayuni wanakiri kuwa wigo wa makundi ya Muqawama umepanuka kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa na hii ni ishara ya kubadilika mlingano wa nguvu kwa manufaa ya Muqawama wa Palestina na kuongezeka uwezo na nguvu za umma katika Ukingo wa Magharibi na Ghaza.

Kuenea mapambano ya wananchi katika Ukingo wa Magharibi ni matokeo ya kushindwa utawala wa Kizayuni kuudhoofisha Muqawama, kuendelea kuwa thabiti nafasi ya makundi ya Muqawama mbele ya umma, kujitokeza makundi mapya yenye kujitegemea na kubadilika mapambano hayo katika sura ya vuguvugu pana la kijamii.

Ungamo la wataalamu na makamanda wa Kizayuni, lenyewe ni ushahidi bora zaidi wa kuthibitisha ukweli kwamba, Muqawama umepata nguvu na ushawishi ambao haujawahi kushuhudiwa. Mwenendo huu unaonyesha kwamba, Ukingo wa Magharibi sasa unabadilika kuwa kitovu na mhimili mpya wa Muqawama wa wananchi ambao kukabiliana nao kutaupa changamoto kali mno utawala wa kizayuni …/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *