Madrid Hispania. Mshambuliaji wa Real Madrid, Kylian Mbappe anaripotiwa atakuwa nje ya uwanja kwa walau wiki tatu, kutokana na jeraha la goti la kushoto.

Mabingwa hao wa LaLiga wamethibitisha kuwa Mbappe amepata majeraha ya kuteguka goti la kushoto, jambo ambalo linaonekana kuwa pigo kubwa kwa timu hiyo.

Mbappe amekuwa kwenye kiwango bora tangu kuanza kwa msimu huu, akifunga mabao 29 na kutoa asisti tano katika mechi 24 alizocheza.

Inaelezwa Mbappe amekuwa akicheza huku akiwa na maumivu ya goti kwa wiki kadhaa zilizopita, lakini kwa mujibu wa tovuti ya L’Equipe, Madrid ilimfanyia vipimo vya MRI Jumatano asubuhi na ikatakiwa atibiwe na apumzike kwa wiki zisizopungua tatu.

Mbappe alifunga katika mechi mbili za mwisho za LaLiga za Madrid dhidi ya Sevilla na Deportivo Alaves, lakini kabla ya hapo hakutumiwa kabisa katika mechi dhidi ya Manchester City.

Katika wiki tatu ambazo Mbappe atakosekana, Madrid itakuwa na mechi mbili za LaLiga dhidi ya Real Betis na Levante, pamoja mechi moja ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Monaco na nusu fainali ya Supercopa de Espana dhidi ya Atletico Madrid.

Vigogo hao kwa sasa wako pointi nne nyuma ya vinara wa LaLiga Barcelona na wanashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kiujumla kwa mwaka jana Mbappe, alifunga mabao 59 kwa mwaka wa kalenda akiwa na Madrid ambapo aliifikia rekodi ya Cristiano Ronaldo iliyodumu tangu 2013.

Kwa sasa pia Mbappe anaongoza orodha ya wafungaji bora wa LaLiga akiwa na mabao 18 ambayo ni sawa na nusu ya jumla ya mabao yote ya Madrid kwenye ligi msimu huu.

 Desemba alifunga hat-trick chini ya dakika saba dhidi ya Olympiacos na alichelewa kwa sekunde 30 kuivunja rekodi ya hat-trick ya haraka zaidi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, inayoshikiliwa na Mohamed Salah aliyoiweka dhidi ya Rangers mwaka 2022.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *