WAZIRI Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema serikali haitakwama kutekeleza miradi mikubwa kwa fedha za ndani kutokana na kasi nzuri ya ukusanyaji wa mapato.
Ameyasema hayo wakati akikagua ujenzi wa Bwawa la Kidunda lililopo mkoani Morogoro wakati alipoanza ziara yake mkoani humo kukagua shughuli za maendeleo.
Dk Mwigulu amesema wote wanaofikiri kuwa serikali itakwama katika kutekeleza miradi yake kwa fedha za Watanzania, basi watakwama wao.
Alieleza kuwa kutokana na ufanisi mkubwa uliooneshwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kusanyaji wa mapato, serikali inawahakikishia Watanzania kuwa hakuna mradi hata mmoja utakaokwama kutokana na kukosekana fedha.
SOMA: Miradi ya kimkakati kuleta neema ya ajira
“Mradi huu na mingine inayoendelea na yenyewe tuiwekee bango kitita katika utoaji wa fedha ili isisimame, ili tufute kabisa katika historia ya mgawo wa maji pale inapotokea ukame na kwa kuwa kazi hii imeshaanza inaonesha uwezo wa kiongozi wetu wa kuona mbali kwa sababu mradi ulianza kabla ya tatizo kujitokeza,” aliongeza.
Alisema hiyo pia inaonesha wazi uwezo wa serikali kuchukua hatua katika kutekeleza na kuyapatia ufumbuzi masuala yanayohusu wananchi na kusisitiza kuwa hilo ni jambo la msingi kufanyika kwa maslahi ya taifa.
Aidha, amemuelekeza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima kuielekeza TRA mkoa huo kuweka bango – mradi utakapokamilika – litakaloonesha kuwa mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 329 umetekelezwa kwa kutumia fedha za Watanzania.
Alisema kwa kufanya hivyo itaupa thamani yake stahiki na pia kuwakumbusha Watanzania kuwa miradi yote inayotekelezwa na serikali yao inatokana na fedha zao na kwamba wana mchango mkubwa katika miradi ya maendeleo.
Aidha, amewataka Watanzania kutumia mifano ya miradi ya Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere pamoja na Bwawa la Kidunda waone kuwa umuhimu wa kulipa kodi na kwamba kulipa kodi ni kwa ajili ya maendeleo yao wenyewe.
Aliongeza kuwa suala la mabadiliko ya tabianchi ni jambo halisia na kwamba Tanzania ardhi haiongezeki lakini watu wake wanaongezeka na shughuli za kijamii na kiuchumi kama kilimo na ufugaji zinaongezeka, na kama taifa litapuuza maonyo yanayotolewa hali itakuwa ngumu zaidi.
“Mtakapokaribia kukamilisha, mkuu wa mkoa waambie Mamlaka ya Mapato Tanzania waje waweke bango kubwa hapa kwamba mradi huu mkubwa umejengwa kwa fedha za walipakodi wa Tanzania ili kuupa thamani mradi huu kwa Watanzania,” alieleza.
Aliwapongeza TRA kwa kuweka rekodi ambayo haijawahi kufikiwa kwa kukusanya Sh trilioni 4.13 kwa mwezi mmoja wa Desemba na Sh trilioni 9.8 kwa miezi mitatu.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa nia yake ya dhati ya kujenga bwawa hilo akisisitiza kuwa mradi huo utasambaratisha mgawo wa maji katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Pia, alimpongeza Waziri Mkuu, Dk Mwigulu kutokana na kujitolea kuwatumikia Watanzania kwa vitendo, akisema kujitolea huko ni ishara tosha kuwa anatekeleza kwa vitendo maelekezo ya Rais Samia.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Malima alisema miradi ya maendeleo mkoani humo inaenda vizuri, na amani na utulivu imetawala.
