JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kuingiza nchini bidhaa za magendo kinyume na sheria ikiwemo vipodozi vyenye viambata vya sumu na mmoja kwa kuingiza nchini trei 48 za mayai ya kuku wa kisasa kutoka Malawi kupitia ‘njia za panya’.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amewataja  watuhumiwa hao kuwa ni Rashidi Mahenge na Said Suleimani, wote wakazi wa Mji Mdogo wa Tunduma mkoani Songwe pamoja na Furaha George.

Amesema Mahenge na Suleimani walikamatwa katika kizuizi cha polisi eneo la Mwakapangala, Kata ya Nsalala, Mji Mdogo wa Mbalizi, kando ya Barabara Kuu ya Mbeya–Tunduma. Amesema watuhumiwa walikamatwa wakiwa wameingiza nchini vipodozi vyenye viambata vya sumu vilivyopigwa marufuku, makasha 22 pamoja na nyavu za kuvulia samaki zilizopigwa marufuku.

Aidha, walikamatwa wakiwa na vitenge jora 42 bila kibali cha kuingiza bidhaa hizo nchini kutoka Zambia kwa kutumia gari aina ya Toyota Mark X lenye namba za usajili T 371 DSS, mali ya Rashidi Mahenge. Kwa upande wake, Furaha George maarufu kwa jina la Mwakatundu mkazi wa Ipyana wilayani Kyela, amekamatwa kwa tuhuma za kuingiza nchini bidhaa bila kibali.

George alikamatwa eneo la Njiapanda ya Kikusya, Kata ya Itope, wilayani Kyela akiwa ameingiza nchini trei 48 za mayai ya kuku wa kisasa pamoja na sukari kilo 40 kutoka Malawi kupitia vivuko visivyo rasmi. SOMA: Dereva, kondakta washikiliwa usafirishaji vipodozi hatari

Wakati huohuo, polisi mkoani Mbeya wanamshikilia Norasco Mgaya mkazi wa Matembwe mkoani Njombe kwa tuhuma za kupatikana na meno mawili ya tembo. Kwa mujibu wa Kamanda Kuzaga, mtuhumiwa huyo alikamatwa eneo la Mafiati Mbeya akiwa na meno hayo yenye uzito wa kilo 1.6 akiwa ameyafunga ndani ya mfuko wa sandarusi na kuyaficha kwenye begi dogo la mgongoni. Amesema mtuhumiwa alisafiri kutoka mkoani Njombe kwa basi la abiria la Kampuni ya Mwendamseke kutafuta wateja kununua meno hayo, lakini alikamatwa kabla hajatimiza azma yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *