Kongwa Aimee ni miongoni mwa wanawake wakimbizi kutoka DRC wanaojitahidi kulea watoto wao peke yao huku wakitegemea msaada wa kibinadamu. Anaelezea changamoto anazokabiliana nazo. 

“Nilikimbia nikiwa na watoto wawili. Baba yao hayupo pamoja nasi na ninawalea peke yangu.” 

Lakini UNFPA sasa imewashika mkono. Akisema kikwembe anaamanisha blanketi, Cotex ni taulo za hedhi na violence economique ni ukatili wa kiuchumi

 “Nashukuru sana. Nilipokea blanketi la kuwafunika watoto wangu wawili, sabuni na mafuta ya kupaka. Pia nashukuru kupokea taulo za kike ambazo nitazitumia wakati wa hedhi. Nashukuru sana kwa msaada mlionipatia.”

UNFPA inasema idadi ya wakimbizi imekuwa ikiongezeka kufuatia wimbi la machafuko DRC.  Dkt. Kacou Pierre Konan, Mratibu wa Programu za UNFPA nchini Burundi anasema.

 “Mwezi Machi 2025 tulipokea wimbi la kwanza la wakimbizi kutoka DRC. Tarehe 5 Desemba tulishuhudia wimbi la pili la waliowasili. Leo hii, kuna takribani wakimbizi 85,000 katika vituo mbalimbali. Tumetembelea vituo vya Ndava na Cishemere kusaidia wanawake na wasichana wakimbizi kwa huduma za afya ya uzazi, vifaa vya kujisafi na vya watoto wachanga.”

Mbali na huduma za afya na misaada ya msingi, elimu kuhusu ukatili wa kijinsia pia inaendelea kutolewa kwa wakimbizi, ili kuwajengea uwezo wa kujilinda na kusaidiana katika jamii. Butoto Veronica,ambaye pia ni  mkimbizi  anasema

“Niliwasili hapa Burundi. Mimi ni mkimbizi kutoka Luvungi, DRC. Shirika lisilo la kiserikali la UPHWO lilinielimisha kuhusu aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia. Nilijifunza kuhusu ukatili wa kiuchumi, jambo ambalo linanisaidia katika familia yangu na katika jamii yangu.”

Hata hivyo, UNFPA inaonya kuwa licha ya msaada unaotolewa na wadau mbalimbali wa kibinadamu, mahitaji ya wakimbizi bado ni makubwa.

“Licha ya juhudi zote zinazofanywa na mashirika mbalimbali ya kibinadamu, yakiwemo ya Umoja wa Mataifa, mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali na yale ya ndani, bado mahitaji ni mengi. Watu wengi wanaishi katika mazingira magumu sana, na takribani asilimia 70 ya wakazi ni watoto, wanawake, wasichana na wavulana wasio na waangalizi. Kwa hiyo, tunatoa wito wa mshikamano huu kuendelea, ili tuweze kusaidia wasichana na na wanawake wajawazito waweze kujifungua katika mazingira salama na yenye utu; kuwasaidia vijana kupata huduma bora; na hasa kuzuia ukatili wa kijinsia au (GBV).”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *