Mohammed Kuno ni kiongozi wa jamii katika eneo la Kasee lililoko kaunti ya Tana River nchini Kenya akieleza hali wanayokabiliana nayo kilasiku. Anasema “Shida ni nyingi sana kwa hapa, hakuna hospitali, shule hakuna, vyanzo vya maji navyo hakuna, hatupati chakula.” 

Wajawazito hapa walikuwa wanakaa muda mrefu bila kujua maendeleo yao kwani ili kupata huduma za afya iliwalazimu kutembea umbali wa kilometa 50 kwenda katika kituo cha afya. Na hali hii ni moja ya sababu za kaunti hii ya Tana River kuwa na idadi kubwa ya vifo wakati wa kujifungua nchini Kenya. 

Wizara ya Afya ya nchini Kenya, uongozi wa Kaunti kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO na wadau wengine wanajitahidi kupatia ufumbuzi tatizo hili kwa kuelekeza nguvu katika kutoa huduma za afya na kipaumbele kinawekwa kwa wajawazito. 

WHO imesaidia katika kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya wa kaunti karibu 170 kwenye masuala kama vile uzazi wa mpango, changamoto wakati wa ujauzito, jinsi ya kumhudumia mtoto mchanga pamoja na kuwahudumia waathirika wa ukatili wa kijinsia. 

Baada ya mafunzo, wahudumu hao wa afya wameweza kuwafikia zaidi ya wananchi 280,000 wa Kaunti ya Tana River tangu mwaka 2024. Mmoja wa wananchi hao ni Madina Musa anayeishi katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Onkolde.

“Wahudumu wa afya wakija hapa wanatusaidia sana, tunapata dawa za watoto na zetu za magonjwa yasiyo makubwa kama vile mafua.”

Mbali na mafunzo WHO pia imetoa vifaa tiba kwa kaunti hiyo vyenye thamani ya dola 574,000 na wahudumu wa afya wanashukuru kwa hilo kama anavyoeleza Ali Ahmed.

“Kwanza mimi nawapongeza na nawapatia asante WHO, nasema nawashukuru pia washirika wote.” 

Kenya inajenga mfumo wa afya madhubuti na unaojibu changamoto za wananchi ili kukabiliana na changamoto na kulinda afya za wananachi wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *