Januari 3 dunia iligubikwa na ripoti za Marekani kushambulia Venezuala na kumtwaa Trump Rais wa nchi hiyo Nicolás Maduro pamoja na mkewe ili wajibu tuhuma dhidi za uhalifu mkubwa dhidi yao nchini Marekani.
Baraza la Usalama, chombo cha Umoja wa Mataifa chenye wajibu wa kusimamia amani na usalama kikatangaza kukutana leo kujikita kwenye suala hilo ambapo hotuba ya Katibu Mkuu Antonio Guterres imesomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Idara ya UN ya masuala ya siasa, (DPPA) Bi. Rosemary DiCarlo ambaye amesema, “Bado nina wasiwasi mkubwa kwamba kanuni za Umoja wa Mataifa hazikuheshimiwa katika shambulizi la kijeshi la tarehe 3 Januari. Chata ya Umoja wa Mataifa inakataza kitisho au matumizi ya nguvu za kijeshi dhidi ya eneo au uhuru wa kisiasa wa taifa lolote.”
Rosemary DiCarlo, Naibu Katibu Mkuu wa Mambo ya Siasa na Ujenzi wa Amani, anazungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali nchini Venezuela.
Wakati huu ambapo Rais Maduro na mkewe wanafikishwa mahakamani leo hapa New York, Marekani Bi. DiCarlo amesema, “Kile ambacho hakina uhakika zaidi ni mustakabali wa sasa wa Venezuela. Nina wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na utulivu nchini humo, madhara yake kikanda, na mfano unaoweza kuwekwa juu ya uhusiano kati ya nchi na vile mataifa yanavyoendeshwa.”
Mgogoro wa sasa unatokea baada ya miaka ya misukosuko, iliyozidishwa na uchaguzi wa rais wa mwezi Julai mwaka 2024 uliobishaniwa ambapo Bi. DiCarlo anasema, “Tumekuwa tukisisitiza uwazi na kuchapishwa kwa matokeo yote ya uchaguzi. Kama tulivyoripoti kwenye Baraza Desemba 23, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, imeorodoshesha ukiukwaji mkubwa.”
Licha ya hali ya sasa Katibu Mkuu kupitia DiCarlo amesema, “natoa wito kwa wana Venezuela wote kushiriki kwenye mazungumzo jumuishi na ya kidemokrasia ambamo kwamo sekta zote za jamii zitaamua mustakabali wao.”
Na zaidi ya yote, “utawala wa sheria lazima uzingatiwe. Sheria ya kimataifa ina mbinu za kutatua masuala kama vile usafirishaji haramu wa dawa za kulevya, mizozo kuhusu rasilimali na masuala ya haki za binadamu.”
Katika mkutano huo, wawakilishi wawili kutoka mashirika ya kiraia watazungumza, ambapo mmoja kaalikwa na Marekani na mwingine amealiwa na Urusi na China.
Jeffrey Sachs ahoji kusiginwa kwa Ibara ya 2 ya Chata ya UN
Baada ya Bi. DiCarlo amefuatia Jeffrey Sachs, Rais wa Mtandao wa Umoja wa Mataifa wa Majawabu ya Maendeleo Endelevu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kituo cha Maendeleo Endelevu katika Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani.
Yeye amesisitiza kuwa suala linalozingatiwa leo si tabia ya Venezuela. “Hoja ni kama nchi mwanachama yeyote ina haki, kwa kutumia nguvu, shinikizo au nugu za kiuchumi, kuamua mustakabali wa kisiasa wa Venezuela au kudhibiti masuala yake ya ndani.”
Baraza linapaswa kuamua kama litalinda au litapuuza Ibara ya 2, kifungu cha 4 cha Chata ya Umoja wa Mataifa inayokataza tishio au matumizi ya nguvu dhidi ya uadilifu wa eneo au uhuru wa kisiasa wa nchi yoyote.
Transparencia Venezuela nayo ‘yaanika’ madhila ya raia
Mercedes De Freitas, Muasisi na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kiraia la Transparencia Venezuela, amelieleza Baraza la Usalama kwamba mashirika ya kihalifu yana “uhusiano wa manufaa” na utawala wa Nicolás Maduro, yakitumia miundo ya serikali kwa biashara ya dawa za kulevya, unyang’anyi na biashara ya binadamu.
Amesema rushwa imekula fedha za umma, na kuwaacha raia wakiwa na huduma duni, ukosefu wa chakula, na unyang’anyi wa kila siku unaofanywa na makundi yenye silaha. “Familia nyingi sana zinategemea mlo mmoja tu kwa siku,” ameonya, akiongeza kuwa kuongezeka kwa kutoadhibiwa kunachochea ukandamizaji, mateso na vifo vinavyosababishwa na ukosefu wa huduma za matibabu — matukio ambayo yameandikishwa na Umoja wa Mataifa.
Akitoa wito wa uwajibikaji, amehimiza kuundwa kwa “serikali iliyo wazi na yenye uwazi” na kuachiliwa huru kwa wafungwa wote wa kisiasa.