Serikali kuwekeza zaidi elimu ujuzi, umahiriSerikali kuwekeza zaidi elimu ujuzi, umahiri

WAZIRI Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika elimu inayojenga umahiri, ujuzi na maadili ili kuwaandaa vijana wenye uwezo wa kufikiri, kubuni na kufanya kazi kwa vitendo.

Alisema hayo wakati akizindua Shule ya Sekondari Chukwani mjini Unguja na kutumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwa maboresho makubwa aliyoyafanya katika sekta mbalimbali ikiwamo elimu.

Alisema maandalizi yanayofanywa kwa vijana hao si kwa ajili ya mitihani pekee, bali kwa kukabiliana na maisha, soko la ajira na kuchangia maendeleo ya taifa.

SOMA: Bilioni 518 kuendeleza elimu Zanzibar

Hivyo alisema serikali itaendelea na ujenzi wa shule za kisasa na utekelezaji wa mtaala mpya pamoja na kuimarisha maandalizi ya walimu na mapitio ya mitaala ili elimu bora ilete tija halisi kwa taifa.

Dk Mwigulu ametoa mwito kwa wananchi, walimu na wanafunzi kwa pamoja waweke kipaumbele katika kulinda, kutunza na kutumia ipasavyo miundombinu ya elimu iliyowekezwa kwa gharama kubwa kwani ni mali ya umma na urithi wa vizazi vya sasa na vijavyo.

Pia, Waziri Mkuu amewasihi wazazi na Watanzania kwa ujumla wajitahidi kulibeba kwa pamoja jukumu la malezi ya vijana.

“Jukumu hili la malezi huanzia nyumbani, ndipo hufikishwa shuleni kwa walimu. Jukumu hili si la walimu pekee, bali ni jukumu letu sote kama jamii,” alisema Dk Mwigulu.

Aidha, alimpongeza Rais Mwinyi akisisitiza: “Ninampongeza Dk Mwinyi kwa ujenzi wa skuli (shule) hizi za kisasa zenye vifaa bora na zilizozingatia matumizi bora ya ardhi kwa ujenzi wa skuli za ghorofa. Elimu ndiyo urithi sahihi, watoto someni kwa bidii na mtumie vizuri fursa hii ambayo serikali imewapatia. Hakikisheni mnaitunza vizuri miundombinu hii”.

Dk Mwigulu amezindua shule hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi kwa vitendo, ambapo alisema wakiweka kipaumbele katika maendeleo ya sekta ya elimu, vijana wa Kitanzania wataweza kujikwamua kiuchumi.

“Ujenzi wa Skuli (shule) hii ya Sekondari ya Chukwani ni mwendelezo wa azma ya serikali ya kujenga skuli za kisasa zinazokidhi mahitaji ya mtaala mpya. Skuli hii ninayofungua leo (jana) imejengwa kwa viwango vya kisasa ikiwa na maabara za sayansi na kompyuta, maktaba na vyumba vya madarasa vinavyowezesha matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika kufundishia na kujifunzia,”alisema Waziri Mkuu.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo inasema ‘Amani na Umoja ndiyo Msingi wa Maendeleo Yetu’, ambayo Waziri Mkuu amesema inaakisi ukweli wa msingi kwamba maendeleo ya taifa lolote hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa amani, utulivu na mshikamano wa wananchi wake.

Alisema kaulimbiu hiyo inawakumbusha wananchi kuwa mafanikio yote wanayoyaona sasa ikiwemo uwekezaji mkubwa katika elimu na miundombinu ya kijamii, yamewezekana kwa sababu ya mazingira ya amani.

“Umuhimu wa kaulimbiu hii uko katika kuhamasisha jamii kuendelea kuilinda na kuienzi amani, kuimarisha umoja wa kitaifa na kushiriki kwa pamoja katika ujenzi wa taifa,” alisema Dk Mwigulu.

Naye Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Khadija Salum Ali alisema serikali imejipanga kuendeleza ujenzi wa shule za kisasa zinazotumia Tehama ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

“Tehama inamwezesha mwalimu aliye popote kuweza kufundisha wanafunzi,” alisema Khadija.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamisi Abdallah Said alisema mradi huo unaohusisha ujenzi miundombinu ikiwamo vyumba vya madarasa 42, ofisi za walimu, maabara na chumba cha kompyuta umegharimu Sh bilioni 6.1 na ulianza Mei 2025 hadi Desemba 2025.

Awali, baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo akiwamo Shekha Hababuu Makame wa kidato cha pili wameishukuru serikali kwa ujenzi wa miundombinu hiyo ambayo itawaongezea ujuzi na maarifa hivyo wameahidi kutoiangusha na badala yake watasoma kwa bidii na maarifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *