MOROGORO: SERIKALI ya Awamu ya Sita itaendelea kuchukua hatua za kuwapelekea wananchi msaada wa kisheria kupitia programu ya Samia legal Aids ikilenga kuwaondolea changamoto za migogoro inayowakabili hususan inayohitaji usaidizi wa kisheria.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Juma Homera amesema hayo Januari 5, 2026, wakati wa ufunguzi wa kliniki ya siku mbili ya msaada wa kisheria mkoani Morogoro katika eneo la stendi ya zamani ya daladala Manispaa ya Morogoro.

Amesema programu ya Samia Legal Aids ilishafanyika mkoani mkoani Morogoro mwaka jana hata hivyo bado kuna uhitaji mkubwa wa wananchi kupata huduma hiyo ili kuondoa changamoto zinazowakabili.
“Kwa sasa Wizara ya Katiba na Sheria iko kwenye maandalizi ya kupeleka huduma ya Samia Legal Aids kwa kila wilaya kwa nchi nzima,” amesema Dk Homera.
Dk Homera amesema jukumu la wizara ni kuwafuata wananchi ili kuwasongezea huduma ya msaada wa kisheria ili waweza kunufaika na serikali yao chini ya Dk Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa huduma hizo zinatolewa bure kwani Rais Dk Samia Suluhu Hassan ameshafuta gharama zote ili kuhakikisha Watanzania wanyonge wanapata haki kuanzia ngazi ya vijiji, mitaa, kata hadi taifa.
Dk Homera amesema katika utekelezaji huo, Wizara itashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), mawakili wa serikali, na Jeshi la Polisi.


Kuhusu usajili wa v yeti vya kuzaliwa amesema uzoefu unaonesha kuna changamoto kubwa katika upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa na kwa kutambua hilo wizara hivi sasa imebadirisha mfumo na kutoa vyeti ndani ya saa 48 baada ya mtu kumaliza usajili .
“ Katika zoezi linalofanyika mkoa wa Morogoro tumeshirikisha wenzetu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili kupata kitambulisho cha Taifa na hatua hii inatokana kuwa NIDA na Wakala wa Usajili ufilisi na Udhamini (RITA) wanafanya kazi pamoja” amesema Dk Homera.
Licha ya hayo amesema kuwa Serikali imejipanga kila wilaya nchini iwe na mwendesha mshtaka wa serikali ili kuondoa kusiwepo na mgongano wa maslahi wakati wa kufanya upelekezi na usikilizwaji wa kesi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, ametoa wito kwa Serikali Kuu kuimarisha na kueneza nchi nzima mfumo wa “Utatu” unaotumiwa mkoani humo katika kushughulikia masuala ya kijinsia na kisheria, kwani umeleta mapinduzi makubwa katika utoaji haki.