Marekani. Msanii wa Hip Hop, mtayarishaji muziki na mwanamitindo kutokea Marekani, Asap Rocky, 37, ametangaza mpango mkubwa wa kurejesha fadhila katika mtaa aliokulia kwa kushirikiana na kampuni ya Bilt.

Kupitia kampeni iitwayo ‘Rent Free’, Asap Rocky na Bilt watagharamia kulipa kodi ya mwezi Januari 2026 kwa wapangaji wote wanaoishi katika jengo alilokulia huko Harlem, New York.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni sehemu ya kusherehekea ujio wa albamu yake ya nne, Don’t Be Dumb ambayo inatarajiwa kutoka mwezi huu chini ya lebo za AWGE, Polo Grounds na RCA.

“Siku zote kwangu imekuwa kuhusu jamii na mtaa wangu wa Harlem ulionifanya kuwa mtu niliye leo, kuanzia uptown hadi downtown,” alisema Asap Rocky na kuongeza.

“Bilt waliposema wanataka kulipia kodi kwa kila mtu katika jengo lilelile nililokulia, hilo lilikuwa jambo la kipekee sana kwangu. Hii sio tu biashara, huo ni uelewa wa maana halisi ya jamii,” alieleza.

Asap Rocky ambaye ni mpenzi wa mwimbaji Rihanna, pia alieleza umuhimu wa albamu yake na mchango huo kwa majirani zake na jamii kwa ujumla.

“Hii ni barua yangu ya upendo kwa New York, na kuweza kuurudishia wema mahali paliponilea ni aina ya ushirikiano ambao una maana ya kweli,” alisema Asap Rocky.

Vinyl anayoizungumzia Asap Rocky, ni aina ya rekodi ya muziki yenye umbo la duara na husifika kwa kutoa sauti ya kipekee zaidi. Ilikuwa maarufu kabla ya ujio wa kanda (cassette), CD n.k.  

Hivyo mbali na kulipia kodi, Asap Rocky amezindua pia toleo maalumu la Vinyl la albamu yake (Don’t Be Dumb), toleo ambalo amelibuni mwenyewe. Na Vinyl hiyo itapatikana kwa wanachama wa Bilt kupitia oda maalumu.

Aidha, Asap Rocky ataonekana kwenye toleo maalum la kipindi cha michezo cha Bilt kiitwacho Rent Free, ambapo wanachama wa Bilt kote Marekani watapata nafasi ya kushinda malipo ya kodi hadi Dola2,500, wastani wa Sh6.1 milioni.  

Washindi 10 wa juu watapata vinyl hiyo ya kipekee ikiwa imesainiwa na Asap Rocky mwenyewe, huku mamia ya wanachama wengine wakipata pointi za ziada za Bilt.

Albamu ya Don’t Be Dumb inatarajiwa kutoka rasmi Ijumaa, Januari 16, 2026, baada ya kuahirisha kwa mara kadhaa. Ingawa orodha rasmi ya nyimbo zake bado haijatolewa, imeripotiwa kuwa wimbo wake, Riot (Rowdy Pipe’n) (2022), huenda ikawa singo ya kwanza ya albamu hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *