Dar es Salaam. Mwimbaji wa Bongo fleva, Barnaba Classic, 35, anatarajia kuachia albamu yake nyingine mwaka huu wa 2026, huku akiwa na kumbukumbu nzuri za mafanikio makubwa aliyoyapata kutoka katika albamu iliyopita.

Kwa hatua hiyo, ni wazi kuwa Barnaba anataka kuweka rekodi nyingine katika Bongo Fleva kama alivyofanya kupitia albamu yake, Love Sounds Different (2022) chini ya Ziiki Media.

Barnaba, mwanzilishi wa High Table Sound, hadi sasa ndiye mwanamuziki aliyetoka chini ya Tanzania House of Talent (THT) ambaye amefanikiwa kutoa albamu na Extended Playlist (EP) nyingi zaidi.

Utakumbuka mbali na Barnaba, waimbaji wengine walioibuliwa na THT ni pamoja na Jay Melody, Mwasiti, Linah, Amini, Ruby, Ibrah Nation, Recho Kizunguzungu, Jolie, Ally Nipishe, Nandy n.k.

Akizungumzia mipango yake kwa mwaka 2026, Barnaba amesema albamu ndio kipaumbele chake na tayari maandalizi yake yameanza tangu kitambo, hivyo kuanzia Januari hii atakuwa katika mchakato wa kumaliza kazi hiyo.  

“Kubwa zaidi, nitatoa albamu yangu ya sita ikiwa imepita miaka mitaatu tangu nilipotoa ‘Love Sounds Different’ iliyotikisa na kufanya vyema sana baada ya nyimbo kama Hadithi, Marry Me, Sayuni, Tamu, Mzuri, Cheketua, n.k,” ameeleza.

“Sasa hii ya sasa itakuwa tishio sana; pengine itakuwa na nyimbo 16. Nimefurahi sana na nilishaanza kuifanyia kazi tangu mwaka 2023. Hivyo kuanzia Januari hii nitakuwa nina vacation nyingi kwa ajili ya finishing, recording na mastering, pamoja na baadhi ya kolabo kubwa kuzikamilisha.”

Hadi sasa baadhi ya albamu alizotoa Barnaba ni pamoja na Gold (2018), Refresh Mind (2020), Love Sounds Different (2022) n.k, huku EP ikiwa ni Mapenzi Kitabu (2020).

“Utofauti ni mkubwa sana: kuanzia ubunifu wa sauti, melodi, kuongeza vionjo vya zamani au kisasa. Lakini hii ni albamu ambayo nina uhakika itakuwa historia. Kwa mara ya kwanza hutajutia kuisikiliza hii albamu,” amesema Barnaba.

Albamu yake ya mwisho kuachia, Love Sounds Different (2022) ambayo mtayarishaji wake mkuu ni mwimbaji mwenzake, Diamond Platnumz, ilifanya vizuri ikishinda tuzo pamoja na kupata mamilioni ya wasikilizaji katika majukwaa ya kidijitali.

Kwa mwaka 2022, ndio albamu ya Bongo fleva iliyotoka ikiwa na idadi kubwa zaidi ya nyimbo, ambazo ni 19 zenye urefu wa saa moja na dakika 4, na huu ni mradi wake wa kwanza kufanya hivyo.

Vilevile ilishirikisha wasanii wengi wenye majina makubwa Afrika Mashariki kama Alikiba, Jux, Diamond, Nandy, Rayvanny, Phina, Jay Melody, Kusah, Young Lunya, Mbosso na Lady Jaydee.

Wengine ni malkia wa taarab, Khadija Kopa, mwimbaji mahiri wa muziki wa Injili, Joel Lwaga, na rapa wa Kenya, Khaligraph Jones, mshindi wa African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) kama Msanii Bora wa Hip Hop Afrika 2018.

Utakumbuka huyu Khaligraph Jones amesikika katika albamu na EP nyingi Bongo, miongoni mwa hizo ni Afro East – 2020 (Harmmize), Only One King – 2021 (Alikiba), Mbuzi – 2024 (Young Lunya) n.k.

Katika Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2022, albamu hiyo ya Barnaba (Love Sounds Different), ilishinda kama Albamu Bora ya Mwaka, ikiwa ni mara yake ya kwanza kushinda kipengele hicho ndani ya TMA.

Ushindi huo ulikuja baada ya kuzibwaga albamu nyingine kali kama ‘The Kid You Know’ ya Marioo, ‘Made For Us’ ya Harmonize, ‘Street Ties’ ya Conboi na ‘Romantic’ ya Kusah.

Hata hivyo, Marioo alilalamika akidai kuwa albamu yake, The Kid You Know (2022) ndio ilistahili ushindi huo, madai ambayo Barnaba aliyajibu kirahisi tu akimtaka Marioo akaichukue hiyo tuzo kama anahisi ilikuwa halali kwake!.

Moja ya nyimbo ambazo kwa mara ya kwanza zilisikika katika albamu hiyo ya Barnaba ni ‘Hadithi’ akimshirikisha Diamond. Ni wimbo ambao hadi sasa video yake imetazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 12.

Na hadi sasa albamu hiyo imesikilizwa (streams) zaidi ya mara milioni 68.8 Boomplay, na kwa ujumla nyimbo zake zote zimefikisha ‘streams’ milioni 104.3, akiwa ni msanii wa tatu kutokea THT kupata namba hizo.

Hivyo albamu mpya ya Barnaba aliyoahidi kuitoa mwaka huu, ni safari nyingine ya kutaka kuweka rekodi katika muziki wake na Bongo fleva kwa ujumla, na itapimwa kulingana na ubora na mafanikio ya ile iliyotangulia.

Ikumbukwe safari ya Barnaba kimuziki ilianza akiwa bado mwanafunzi, alikuwa akienda THT na nguo za shule ili kutafuta njia ya kuonyesha kipaji chake cha uimbaji.

Wakati huo Mwasiti ndiye aliyekuwa Jaji wa THT na alimpa nafasi hadi kuja kutoka, na baadaye Barnaba alimwandikia Mwasiti wimbo wake maarufu, Sio Kisa Pombe (2011) akimshirikisha Quick Rocka.  

Ikumbukwe Mwasiti yeye alitangulia kutoka kimuziki kupitia wimbo wake, Niambie (2006) uliofanya vizuri hadi akashinda tuzo ya TMA kama Msanii Bora Chipukizi akiwa msanii wa kwanza wa THT kubeba tuzo hiyo.

Na huyu Mwasiti aliyeanza kujihusisha na muziki akiwa na miaka tisa tu mwaka 1995, ndiye msaniii wa kwanza wa kike Bongo kutajwa kuwania vipengele vitano katika tuzo za TMA, hiyo ilikuwa 2013.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *