Katika maisha ya ukocha, kuna msemo maarufu zaidi unaosema ‘Makocha huajiriwa ili kufukuzwa.’ Hii inamaanisha kwamba, kocha anapopewa dili la kufundisha timu fulani, kichwani kwake aweke kwamba ipo siku isiyo na jina ataondoka kwa kufukuzwa. Wachache sana huondoka wenyewe iwe kwa kustaafu au kupata dili kwingine.
Katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara 2025-2026, hadi sasa zikiwa zimepigwa mechi za raundi 10, huku baadhi ya timu zikiwa na viporo kibao hadi vitano, kuna makocha saba tulioanza nao lakini sasa hawapo.
Sababu mbalimbali zimetajwa kuondoka kwa makoch hao ikiwa ni takribani miezi mitatu katika kipindi cha Septemba 17, 2025 ligi ilipoanza hadi Desemba 7, 2025 iliposimama kupisha AFCON.
Romain Folz (Yanga)
Mfaransa huyu alitua Yanga Julai 14, 2025, akaondoka Oktoba 31, 2025, akikaa kwa takribani miezi mitatu. Mechi sita pekee alikaa kuiongoza Yanga zikiwamo mbili za ligi dhidi ya Pamba Jiji ambayo Yanga ilishinda 3-0 na Mbeya City zikitoka 0-0.
Nyingine ya Ngao ya Jamii, Yanga ikiifunga Simba 1-0. Upande wa kimataifa, Folz aliiongoza Yanga kuifunga Wiliete nje ndani kwa ushindi wa 3-0 na 2-0, kisha akasitishiwa mkataba baada ya kichapo cha 1-0 kutoka kwa Silver Strikers.
Kitendo cha Yanga kufungwa ugenini na Silver Strikers hali iliyohatarisha kupoteza nafasi ya kufuzu makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, ikahitimisha safari yake. Kwa sasa nafasi yake imechukuliwa na Pedro Goncalves.
Fadlu Davids (Simba)
Alikuwa na Simba tangu msimu uliopita ambapo Msauzi huyo alitua Julai 5, 2024. Aliifikisha Simba fainali ya Kombe la Shirikisho 2024-2025 na kupoteza kwa jumla ya mabao 3-1 dhidi ya RS Berkane.
Septemba 21, 2025, akaandika barua ya kusitisha mkataba baada ya kupata dili la kuinoa Raja Casablanca ya Morocco alipo sasa ambapo awali alikuwa msaidizi kikosini hapo kabla ya kutua Simba, hivyo amerejea alipotoka.
Fadlu msimu huu aliiongoza Simba katika mechi mbili pekee za mashindano, akianza na kichapo cha 1-0 dhidi ya Yanga kwenye Ngao ya Jamii, kisha ushindi wa 1-0 ugenini kwa Gaborone United ikiwa ni Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali.
Alipoondoka, mrithi wake akawa Dimitar Pantev ambaye alikuwa akiinoa Gaborone.
Dimitar Pantev (Simba)
Katika listi hii, Simba ndiyo timu iliyoachana na makocha wawili katika kipindi cha miezi hiyo mitatu. Hakuna nyingine iliyofanya hivyo.
Pantev hakudumu sana Msimbazi, kwani aliporithi mikoba ya Fadlu, Oktoba 6, 2025, akaondoka Desemba 2, 2025. Ni takribani miezi miwili pekee imetosha kuwa familia ya Simba.
Katika kipindi hicho, aliiongoza Simba kucheza mechi tano ikiwamo moja ya Ligi Kuu katika ushindi wa 2-1 dhidi ya JKT Tanzania na nne za Ligi ya Mabingwa akianza na ushindi wa 3-0 dhidi ya Nsingizini Hotspurs ugenini, kisha nyumbani akalazimishwa 0-0, akaipeleka Simba makundi.
Hatua ya makundi, vichapo viwili mfululizo kutoka kwa Petro Atletico (1-0) na Stade Malien (2-0), vikiifanya Simba kuburuza mkia wa kundi D, vimemuondoa kocha huyo raia wa Bulgaria.
Pantev ameondoka Simba na bado hana timu, lakini mrithi wake klabuni hapo amepatikana ni Steve Barker raia wa Afrika Kusini akitokea Stellenbosch.
Marcio Maximo (KMC)
Heshima aliyoiweka akiwa Taifa Stars wakati alipokuja mara ya kwanza Tanzania 2006 hadi 2010, ameshindwa kuiweka upande wa klabu kwani mara zote aliporejea nchini kuinoa Yanga (2014) na KMC (2025), hakuondoka vizuri. Rekodi zimemkataa.
Akiwa Taifa Stars, aliipeleka timu kushiriki fainali za kwanza za CHAN 2009 nchini Ivory Coast.
Maximo katika kipindi cha Agosti 1, 2025 hadi Desemba 1, 2925 akiwa na KMC, alianza msimu kibabe kwa ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji.
Mechi hiyo iliyochezwa Septemba 17, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, ndio pekee kwa Maximo na jeshi hilo la Vijana wa Kino kutoka na ushindi uwanjani.
Mara baada ya mechi hiyo, KMC chini ya Maximo haikuonja tena ushindi wowote zaidi ya vipigo sita mfululizo, kisha kujitutuma mbele ya Mtibwa Sugar kwa kutoka nao suluhu kabla ya kupasuka mechi ya tisa ikiwa ugenini jijini Mwanza dhidi ya Pamba Jiji na kuwa tiketi ya kocha huyo kusitishiwa mkataba, akiwa ameiacha timu mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikivuna pointi nne tu katika mechi tisa, ikishinda mechi moja, kupoteza saba na kutoka sare moja.
Huwezi kuamini, lakini ndiyo ukweli ulivyo. KMC ya Maximo katika mechi tisa ilizocheza, ilivuna mabao mawili tu, yote yakifungwa na Daruwesh Saliboko. Alifunga katika mechi ya kwanza nyumbani dhidi ya Dodoma Jiji na siku ilipofumuliwa mabao 4-1 na watetezi Yanga kwenye Uwanja wa KMC, washindi wakiwa wenyeji na kuifanya timu hiyo na wastani wa 0.2 kwa kila mechi.
KMC ya Maximo, ilicheza mechi nne za ugenini na zote imepasuka, ikifunga bao moja tu na yenyewe kufungwa jumla ya mabao tisa.
Ilianza kucheza ugenini dhidi ya Maafande wa Tanzania Prisons na kulala 1-0 kabla ya kuifuata Fountain Gate mjini Babati na kulala pia 1-0.
Baada ya hapo ikavaana na Yanga, iliyowafumua mabao 4-1 kabla ya Pamba Jiji kuwanyoosha 3-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jiji Mwanza.
Licha ya kuanza na mguu mzuri kwa ushindi katika mechi ya kwanza ikiwa uwanja wa nyumbani, KMC ya Maximo ilionekana pia nyonge hata ikicheza Uwanja wa KMC, kwani ilipoteza mechi zote tatu zilizofuata kabla kuibana Mtibwa Sugar katika mechi ya mwisho ikiwa KMC Complex kwa kuambulia suluhu.
KMC ilianza gundu la nyumbani katika mechi ya pili tu ya msimu huu dhidi Singida Black Stars kwa kulala bao 1-0 kabla Mbeya City kuitia aibu kwa kipigo cha mabao 3-0. Mechi ya nne nyumbani ilikuwa ni dhidi ya Yanga na kugongwa 4-1 safi, ndipo ikaja ikatoka suluhu na Wakata Miwa wa Manungu.
Takwimu zinaonyesha katika mechi tano za nyumbani, KMC ya Maximo ilivuna pointi nne na bao moja na kufungwa matano na kuwa angalau kidogo kwa kulinganisha na mechi za ugenini ambazo haikupata hata pointi moja, lakini ilibahatika kufunga bao moja pia.
Mara baada ya kutemeshwa kibarua, Maximo alisema, licha ya yaliyotokea lakini kwake ameyapokea kwa sababu bado kwa taaluma suala la kuondoka sehemu moja kwenda nyingine ni la kawaida na yupo kiroho safi.
“Ni fahari kwangu kufanya kazi Tanzania kwa sababu ni nchi ninayoipenda, watu wake wanapenda mpira na kiukweli nimeona tangu mara ya kwanza nakuja hapa, Ligi Kuu imepiga hatua, ndiyo maana ni kivutio cha makocha wengi pia,” alinukuliwa Maximo.
Maximo bado hana timu, mrithi wake pale KMC ni Abdallah Mohamed Baresi aliyetokea Zimamoto ya Ligi Kuu Zanzibar.
Malale Hamsini (Mbeya City)
Aliitumikia Mbeya City kwa takribani miezi minane kwani alitua Machi 31, 2025 wakati timu inashiriki Ligi ya Champioship, akichukua mikoba ya Salum Mayanga, akafanikiwa kuipandisha daraja.
Kocha huyo ameondoka Mbeya City Novemba 30, 2025 baada ya kuiongoza katika mechi tisa za Ligi Kuu Bara, akishinda mbili dhidi ya Fountain Gate (1-0) na KMC (3-0), akapoteza tano dhidi ya Azam (2-0), Tanzania Prisons (2-1), Mashujaa (1-0), Coastal Union (2-0) na Namungo (1-0). Sare ni dhidi ya Yanga (0-0) na JKT Tanzania (2-2).
Kwa sasa Malale anainoa KVZ inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar, huku Mecky Maxime akichukua nafasi yake pale Mbeya City.
Denis Kitambi (Fountain Gate)
Baada ya kutoonekana na kikosi cha Fountain Gate katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa Septemba 28, 2025 kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, taarifa zilibainisha, Kitambi amemalizana na uongozi wa klabu hiyo huku sababu ya kufanyika hayo ikiwekwa wazi.
Kitambi aliyeonekana kwa mara ya kwanza akikiongoza kikosi hicho Agosti 31, 2025 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Tabora United, huku akitambulishwa rasmi Septemba 20, 2025, amefanikiwa kuiongoza Fountain Gate katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara na kupoteza zote dhidi ya Mbeya City (1-0) na Simba (3-0).
Ilielezwa Kitambi alifikia makubaliano ya kuachana na Fountain Gate kutokana na sababu zake binafasi.
Fountain Gate haikuanza msimu vizuri kufuatia kukumbana na changamoto kwenye mfumo wa usajili ambapo ilikuwa na wachezaji 14 pekee waliofanikiwa kusajiliwa kwa wakati ambao ndiyo waliohusika kwenye mechi ilizocheza chini ya Kitambi hadi pale baadae mambo yalipokaa sawa, wakaongeza wengine.
Hali hiyo inatajwa kuwa ndiyo miongoni mwa sababu za Kitambi kuishia njiani kwani licha ya timu kucheza vizuri, lakini ilikumbana na changamoto hiyo.
Baada ya Kitambi kuondoka, kikosi hicho kinaongozwa na Mohamed Ismail ‘Laizer’ ambaye awali alikuwa msaidizi hapo.
Ali Mohammed Ameir (Coastal Union)
Oktoba 1, 2025, Coastal Union ilitangaza kusitisha mkataba wa kocha huyu aliyetua kikosini hapo msimu huu. Nafasi yake imechukuliwa na Mohamed Muya.
Taarifa ya kusitisha mkataba wa Ameir kutoka Coastal Union ilisema: “Uongozi wa Klabu ya Mpira wa Miguu ya Coastal Union umefikia makubaliano ya pande zote ya kusitisha kandarasi na kocha mkuu Ali Mohammed Ameir.
“Klabu inamshukuru mwalimu Ali Mohammed Ameir kwa mchango wake uliotukuka kwa kipindi chote alichoiongoza timu yetu.
“Uongozi wa Coastal Union utaujulisha umma juu ya muundo na uongozi mpya wa benchi la ufundi muda mchache ujao.”
Ameir aliiongoza Coastal katika mechi tatu za Ligi Kuu Bara msimu huu akishinda moja dhidi ya Tanzania Prisons (1-0), kisha kupoteza 2-1 mbele ya JKT Tanzania na kulala 2-0 kwa Dodoma Jiji.
Mara baada ya vipigo hivyo, zilienea tetesi kwamba mabosi wa klabu hiyo walikuwa mbioni kumpiga chini na baadaye ikawa kweli kutokana na Coastal Union kutangaza rasmi Oktoba Mosi 2025.