Ikumbukwe kuwa miaka 80 iliyopita baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, mataifa 50 yalikutana huko San Francisco hapa nchini Marekani na kupitisha Chata iliyoanzisha Umoja wa Mataifa. Miongoni mwa malengo ni kuzuia vita na kujenga uhusiano mwema baina ya mataifa. Mathalani kuepusha nchi moja kuvamia nchi nyingine na kulinda haki za binadamu. 

Leo hii Chata hiyo imeendelea kusiginwa na kilichoibua mjadala zaidi ni tukio la Januari 3 la Vikosi Maalum vya Marekani kuingia Venezuela na kumtwaa Rais wa nchi hiyo Nicolas Maduro pamoja na mkewe kwa madai ya kwamba wanatakiwa wajibu tuhuma nchini MArekani za uhalifu mkubwa ikiwemo usafirishaji wa dawa za kulevya.

Chata ya Umoja wa Mataifa ina sura 19 lakini tunamulika sura mbili tu ambazo zinaangazia masuala ya amani na usalama. Na ifahamike kuwa chombo cha Umoja wa Mataifa kinachowajibika na amani na usalama ni Baraza la Usalama lenye wajumbe 15, ambapo watano ni wa kudumu nao ni Marekani, China, Urusi, Ufaransa, na Uingereza, wote wakiwa na kura turufu au veto inayoweza kuzuia hoja yoyote Barazani.

Sura ya kwanza ya Chata ya UN

Nianze na Sura ya Kwanza inayomulika Malengo na Kanuni. Miongoni mwa malengo hayo ni Kudumisha amani na usalama wa kimataifa, na kwa madhumuni hayo: kuchukua hatua za pamoja zilizo madhubuti kwa ajili ya kuzuia na kuondoa vitisho dhidi ya amani, na kukandamiza vitendo vya uchokozi au ukiukaji mwingine wa amani, na kufanikisha kwa njia za amani, na kwa kuzingatia kanuni za haki na sheria ya kimataifa, marekebisho au usuluhishi wa migogoro au hali za kimataifa ambazo zinaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Chata imeweka na kanuni katika Ibara ya 2 inayosema kuwa  Shirika na wanachama wake, katika kutekeleza malengo kwa mujibu wa Ibara ya 1 lazima lizingatie kanuni ikiwemo kifungu kidogo cha 4 kinachosema kwamba, Wanachama wote watajiepusha, katika uhusiano wao wa kimataifa, na tishio au matumizi ya nguvu dhidi ya uadilifu wa eneo au uhuru wa kisiasa wa nchi yoyote, au kwa namna nyingine yoyote isiyolingana na Malengo ya Umoja wa Mataifa.

Uamuzi ni wa Baraza la Usalama

Na iwapo kuna hali yoyote tata Baraza la usalama ndio la kuamua matumizi ya kijeshi kama isemavyo Sura ya 7 Ibara ya 39 kwamba, Baraza la Usalama litaamua uwepo kwa tishio lolote dhidi ya amani, uvunjifu wa amani, au kitendo cha uchokozi, na litatoa mapendekezo, au kuamua ni hatua zipi zitachukuliwa kwa mujibu wa Ibara ya 41.

Na je Ibara hiyo inasemaje? Ibara ya 41 inasema kwamba Baraza la Usalama linaweza kuamua ni hatua zipi zisizohusisha matumizi ya nguvu za kijeshi zitumike ili kutekeleza maamuzi yake, na linaweza kuwaomba Wanachama wa Umoja wa Mataifa watekeleze hatua hizo. Hatua hizo zinaweza kujumuisha kusitishwa kabisa au kwa sehemu kwa mahusiano ya kiuchumi, pamoja na usafiri wa reli, baharini na angani, huduma za posta, telegrafu, redio, na njia nyingine za mawasiliano, na pia kukatwa kwa mahusiano ya kidiplomasia.

Nguvu za kijeshi zinatumika wakati gani?

Na vipi hatua hiyo ikionekana haitoshelezi? Hapo ndipo ibara ya 42 ya sura 7 ya Chata itatumika kuhusu nguvu za kijeshi ikisema, , linaweza kuchukua hatua kwa kutumia majeshi ya anga, baharini, au nchi kavu kadiri itakavyohitajika ili kudumisha au kurejesha amani na usalama wa kimataifa. Hatua hizo zinaweza kujumuisha maonyesho ya nguvu, vizuizi (blockade), na operesheni nyinginezo zinazofanywa na majeshi ya anga, baharini, au nchi kavu ya Wanachama wa Umoja wa Mataifa.”

Kundi la Marafiki la Kulinda Chata ya Umoja wa Mataifa lapaza sauti

Na ndipo kwenye mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Januari 5, 2026 kuhusu tishio la amani na usalama, suala la Chata ya Umoja wa Mataifa kusiginwa baada ya Marekani kuingia Venezuela likawekwa bayana na Kundi la Marafiki la Kulinda Chata ya Umoja wa Mataifa. Hotuba yao iliwasilishwa na Mwakilishi wa Kudumu wa Eritrea kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Sophia Tesfamariam Yohannes. Eritrea ni mmoja wa wanachama 18 wa kundi hilo lililoanzishwa mwaka 2021.

Balozi Sophia amesema, “vitendo vya aina hiyo vinakiuka sheria ya kimataifa na kila kanuni inayosimamia uhusiano wa kimataifa, ikiwemo yale yaliyoainishwa kwenye Chata ya Umoja wa Mataifa.”

Na kisha akatamatisha kwa kusema,“nchi Wanachama wa Kundi la Marafiki la Kulinda Chata ya Umoja wa Mataifa zinatoa wito kwa vyombo vyote husika vya kimataifa, ikiwemo Baraza la Usalama na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kuchukua hatua za haraka ili kulinda malengo na kanuni zilizoainishwa katika Chata ya Umoja wa Mataifa, na kuchukua kwa dharura hatua zinazofaa ili kuepusha kuongezeka zaidi kwa hali ilivyo katika eneo husika, hasa vitendo vya ziada vya uchokozi dhidi ya mamlaka na uhuru wa eneo la Venezuela, na kulinda amani na usalama wa kikanda na kimataifa.”

‘Mpini wa kisu cha amani’ wameshikilia nchi wanachama – Guterres

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani, Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric aliulizwa kwa usiginaji huu wa Chata, je Umoja wa Mataifa umepoteza umuhimu na unakabiliwa na sintofahamu ya utambulisho na utekelezaji wa majukumu yake kwani unashindwa kusongesha ajenda  ya dunia huku mataifa yenye kura turufu barazani yakifanya  vile watakavyo?

Jibu la Dujarric ni kwamba, “Utambulisho wetu umejikita katika Chata, katika sheria za kimataifa, na katika Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu. Kuna swali halali la kuyauliza mataifa wanachama jinsi yanavyoheshimu na kutekeleza sheria na mikataba ambayo wao wenyewe wameweka. Pia kuna swali halali, ambalo Katibu Mkuu mwenyewe amelisisitiza, kwamba sheria za kimataifa na Mkataba si menyu ya kuchagua vipengele unavyotaka; ni mfumo mzima. Mataifa wanachama yaliunda shirika hili ili kuokoa vizazi vijavyo dhidi ya janga la vita. Tunahitaji mataifa wanachama yalinde na kuendeleza shirika hili na maadili yake kwa ajili ya manufaa ya vizazi vijavyo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *