Denmark na Greenland zinataka kuwa na mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, kufuatia msimamo mkali wa utawala wa Rais Donald Trump unaosisitiza nia ya Marekani kuichukua Greenland, kisiwa cha kimkakati kilichopo eneo la Aktiki kinachomilikiwa na Denmark.
Mvutano uliongezeka baada ya Ikulu ya White House kusema Jumanne kuwa “chaguo la kijeshi la Marekani liko mezani,” kauli iliyokosolewa vikali na viongozi kadhaa wa Ulaya waliopinga wito wa Trump, wakisisitiza maslahi ya kimkakati ya eneo hilo.
Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, alionya kuwa hatua kama hiyo itaashiria mwisho wa muungano wa kijeshi wa NATO. Wachambuzi wanasema kauli za Trump zinahatarisha uhusiano wa washirika.
Kauli za Trump zakemewa vikali na viongozi duniani
Viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Italia, Poland, Hispania na Uingereza wameungana kusisitiza kuwa Greenland ni mali ya watu wake.