Kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na Idara ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (DESA), kupungua kunatokana na migogoro inayoendelea ya kibiashara, mivutano ya kisiasa na kijiografia, na misukosuko ya kifedha inayochochewa na mzigo mkubwa wa madeni.
Ikipatiwa jina Hali ya Uchumi na Matarajio ya Dunia ya mwaka 2026 (WESP 2026), ripoti inaonesha kuwa mwaka 2025, katika hali isiyotarajiwa uchumi wa dunia ulihimili mitikisiko iliyosababishwa na Marekani kuongeza ushuru licha ya kwamba bado kuna udhaifu ikiwemo, uwekezaji mdogo na nafasi finyu ya kifedha kwa serikali unaendelea kudhoofisha kasi ya ukuaji.
“Kupungua kidogo kwa mivutano ya kibiashara kulipunguza kuvurugika kwa biashara ya kimataifa. Hata hivyo athari mbayá za viwango vya juu vya ushuru vilivyowekwa na Marekani pamoja na sintofahamu kwenye uchumi mkuu inatarajiwa kuwa dhahiri zaidi mwaka huu wa 2026,” imesema ripoti hiyo.
Watu wakinunua bidhaa katika kituo cha ununuzi huko Japani.
Kauli ya Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amenukuliwa katika taarifa hiyo akisema kuwa, “mchanganyiko wa mivutano ya kiuchumi, kijiografia na kiteknolojia inabadilisha hali ya kimataifa, na kusababisha kutokuwa na uhakika mpya wa kiuchumi na kudhoofisha jamii. Nchi nyingi zinazoendelea kiuchumi zinaendelea kutatizika na, kwa sababu hiyo, maendeleo kuelekea Malengo ya Maendeleo Endelevu yanasalia mbali kwa sehemu kubwa ya dunia.”
Afrika: Mfumuko wa bei unapungua lakini bei ziko juu
Wataalamu wa uchumi kutoka DESA wanakadiria kuwa ukuaji wa uchumi barani Afrika utaongezeka kidogo hadi asilimia 4.0 mwaka 2026.
Hata hivyo, wanaonya kuwa mzigo wa madeni na majanga ya tabianchi bado ni vikwazo vikubwa kwa maendeleo ya bara hilo.
Ingawa mfumuko wa bei unatarajiwa kupungua hadi asilimia 3.1 mwaka 2026, Li Junhua, Mkuu wa DESA amesisitiza kuwa bei za bidhaa bado ziko juu kwa wananchi wa kawaida.
“Hata mfumuko wa bei unapopungua, bei zinabaki kuwa juu na kadri zinavyoendelea kupanda zinaathiri vibaya uwezo wa ununuzi kwa watu walio katika mazingira hatarishi. Ili kuhakikisha kwamba mfumuko wa bei wa chini unatafsiriwa kuwa maboresho halisi kwa kaya, kunahitaji kulinda matumizi muhimu, kuimarisha ushindani wa soko, na kukabiliana na vichochezi vya majanga ya mfumuko wa bei yanayojirudia.”
Wito wa hatua za pamoja
Ripoti ya DESA inahitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa kupitia “Makubaliano ya Sevilla” ili kurekebisha muundo wa fedha wa kimataifa na kusaidia nchi zinazoendelea kupata ufadhili wa maendeleo.
Inabainisha kuwa kukabiliana na kipindi cha mabadiliko ya miungano ya biashara, shinikizo endelevu la bei, na mishtuko inayohusiana na mabadiliko ya tabianchi kutahitaji uratibu wa kina zaidi wa kimataifa na hatua za pamoja zilizo thabiti, wakati ambapo mvutano wa kijiografia unaongezeka, sera zinazidi kuwa za kujielekeza kitaifa, na msukumo kuelekea suluhu za kimataifa za pamoja unapungua.
“Maendeleo endelevu yatategemea kujenga upya imani, kuimarisha uthabiti na kuhuisha dhamira ya mfumo wa biashara wa kimataifa ulio wazi, unaoongozwa na kanuni na sheria,” imesema ripoti hiyo.