Katika taarifa yao iliyotolewa hii leo jijini Geneva Uswisi ujumbe huo umeeleza kuwa wakati maandamano yanavyoingia wiki ya tatu, wana wasiwasi mkubwa kuhusu matumizi ya nguvu kupita kiasi, ukiwataka vyombo vya dola kuzingatia sheria za kimataifa za haki za binadamu. 

Ujumbe huo pia umeeleza kuwa kuna taarifa za kuaminika kwamba Baraza Kuu la Usalama wa Taifa lilitoa agizo la kufanya operesheni “ya maamuzi” bila kuzingatia kujizuia, jambo linaloongeza hatari kwa raia.

Katika wiki mbili zilizopita, kumekuwepo ongezeko la vurugu, huku intaneti ikizimwa na mawasiliano kukatwa kabisa kuanzia jioni ya tarehe 8 Januari. 

Ujumbe huo unaitaka Iran kuheshimu haki ya kukusanyika kwa amani na uhuru wa kujieleza, na kuwaachia huru bila masharti watu wote waliokamatwa kiholela kwa kutumia haki zao za msingi.

Chanzo ni nini?

Maandamano haya yalianza tarehe 28 Desemba 2025 kufuatia kuporomoka kwa ghafla kwa sarafu ya taifa hilo na sasa maandamo hayo yamesambaa katika angalau miji 46. 

Hadi tarehe 7 Januari, 2026 zaidi ya watu 40, wakiwemo angalau watoto watano, waliripotiwa kuuawa katika mikoa kadhaa. Mamia ya waandamanaji na wapita njia, wakiwemo angalau watoto 113, wamekamatwa.

Ujumbe huo wa kusaka ukweli nchini Iran umeonya kuwa ukandamizaji huu unafanana na mifumo ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ulioshuhudiwa wakati wa harakati za “Mwanamke, Maisha, Uhuru”, na kusisitiza kuwa raia wa Iran wanastahili kuishi kwa usalama, heshima na bila hofu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *