Arusha. Wanariadha wa Tanzania wameshindwa kwenye mashindano ya mbio za nyika za dunia ambazo zimefanyika leo Tallahassee, Florida nchini Marekani.

Katika mbio hizo Tanzania iliwakilishwa na wanariadha tisa, watano upande wa mbio za wanaume, kilometa 10 (senior men) na wanne mbio za kupokezana kwa wanaume na wanawake (mixed relay), ambapo imeshuudiwa wanariadha wa Australia, Uganda, Ethiopia, Kenya na Ufaransa wakitawala na kunyakua medali zote, huku Watanzania wakiwa wasindikizaji.

Wanariadha, Daniel Sinda, Elizabeth Ilanda, Ambrosi Amma na Regina Mpigachai wa Tanzania, walitumia muda wa dakika 24:11, kumaliza nafasi ya 11, upande wa mbio za kupokezana kwa wanaume na wanawake (mixed relay).

Austalia ikitamba katika mbio hizo kwa kutwaa medali ya dhahabu, ambapo timu yake ilikuwa inaundwa na Olli Hoare, Linden Hall, Jack Anstey na Jessica Hull ilikimbia kwa nguvu na umakini mkubwa, na kufanikiwa kumaliza kwa dakika 22:23, ikiboresha medali ya shaba waliyoipata mwaka 2023.

Nafasi ya pili, imekwenda kwa ufaransa, ya tatu Ethiopia, huku Kenya, mabingwa mara nne wa mashindano hayo, ikimaliza nafasi ya nne na kukosa medali.

Upande wa wanaume (senior men), Km 10, Tanzania iliwakilishwa na nyota watano, Gabriel Geay, Benjamin Fernandi, Emmanuel Dinday, John Wele na Inyasi Sule, ambapo licha ya kukosa medali, kwenye matokeo ya jumla wameifanya nchi kumaliza nafasi ya sita.

Katika mbio hizo za Km 10, imeshuudiwa nyota Jacob Kiplimo wa Uganda akitwaa medali ya dhahabu baada ya kumaliza wa kwanza kwa muda wa 28:18 huku akiingia kwenye rekodi ya mwanariadha wan ne kushinda mbio hizo mara tatu, nyota wengine ambao wamewahi kufanya hivyo ni John Ngugi, Paul Tergat na Kenisa Bekele.

Medali ya fedha ikaenda kwa Muethiopia Berihu Aregawi kwa 28:36 na Daniel Ebenyo kutoka Kenya akamaliza wa tatu kwa 28:45.

Upande wa wanawake Agnes Ngetich wa Kenya amemaliza wa kwanza kwa dakika 31:28, Joe Shptwick wa Uganda wa pili kwa 32:10 na Sinait Gachio wa Ethiopia akamaliza wa tatu kwa dakika 32:13.

Mbio za vijana chini ya umri wa miaka 20, Wanaume Km8, medali zote zimekwenda Kenya, Frankline Kibet akimaliza wa kwanza kwa 23:18, akifuatiwa na Emmanuel Kiprimo aliyetumia dakika 23:20 na Andrew Alamasi aliyemaliza kwa 23:28.

Wasichana, Km 6, medali ya dhahabu imekwenda kwa Marta Alemayo wa Ethiopia aliyemaliza wa kwanza kwa kutumia dakika 18:52, nafasi ya pili Muethiopia mwenzake Wosane Asefa kwa 9:18 na Mganda Charity Chepkirui akamaliza wa tatu kwa 18:19.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *