Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi amesema hivi leo kuwa kwa sasa “hali imedhibitiwa kikamilifu” nchini humo, hii ikiwa ni baada ya mamlaka kuendesha vitendo vya ukandamizaji. Bila kutoa ushahidi wowote, Araghchi amesema maandamano hayo “yaligeuka kuwa ya  vurugu na umwagaji damu  ili kutoa kisingizio” kwa Rais wa Marekani Donald Trump kuingilia kati.

Trump amesema Iran iko tayari kufanya mazungumzo na Marekani baada ya tishio la kuishambulia kutokana na ukandamizaji huo. Araghchi aliijibu kauli hiyo ya Trump alipokuwa akizungumza na wanadiplomasia mjini Tehran, na kusisitiza kuwa Iran iko tayari kwa mazungumzo lakini pia imejiandaa kikamilifu kwa vita.

Kauli hizo zimetolewa huku wanaharakati wakitahadharisha kuwa kitendo cha serikali kuzima intaneti kwa zaidi ya siku tatu, kimewezesha kuficha vitendo vya ukandamizaji na mauaji dhidi ya waandamanaji hasa wakati huu kukiripotiwa kuwa watu zaidi ya 540 wameuawa katika wiki mbili za maandamano.

Uungwaji mkono, ukosoaji na wito wa amani

Mamlaka za Iran zimekosolewa vikali kutokana na ukandamizaji huo. Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amesema hatua za serikali ya  Iran  dhidi ya waandamanaji zinadhidihirisha “udhaifu wao” na kutaka vurugu hizo kusitishwa. Canada imesema inasimama bega kwa bega na raia wa Iran huku viongozi kadhaa wa Israel akiwemo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wakitangaza kuwaunga mkono waandamanaji.

Beijing | Mao Ning, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China
Mao Ning, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China akizungumza na waandishi wa habari mjini BeijingPicha: Johannes Neudecker/dpa/picture alliance

China kwa upande wake imetoa wito wa “amani”  kama alivyoeleza Mao Ning, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China akisema kuwa wanatumai kuwa serikali ya Iran na watu wake wataweza kuzishinda changamoto za sasa zinazowakabili na watadumisha utulivu katika taifa hilo.

China imesisitiza kuwa inakemea vitendo vyovyote vya uingiliaji wa mambo ya ndani ya Iran na kuwa uhuru na usalama wa nchi zote unapaswa kulindwa kikamilifu na sheria za kimataifa.

“Tunapinga matumizi ya nguvu au tishio la matumizi ya nguvu katika mahusiano ya kimataifa. Tunatoa wito kwa pande zote kuchukua hatua zinazochangia kuleta amani na utulivu huko Mashariki ya Kati,”  alisema Mao Ning.

Aidha, Iran imetoa wito kwa wafuasi wake kuandamana hii leo ili kuunga mkono utawala wa kidemokrasia chini ya Kiongozi Mkuu mwenye umri wa miaka 86 Ayatollah Ali Khamenei. Wakati huo huo, Televisheni ya serikali ya Iran ilipeperusha hewani nyimbo za wafuasi hao wa serikali zilizokuwa zikiyalaani mataifa ya Marekani na Israel.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *