KAGERA: SERIKALI imetenga zaidi ya Sh bilioni 45 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja matano ya kudumu mkoani Kagera ambayo awali yaliharibiwa na mvua za masika na kusababisha changamoto kubwa.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kagera, Mhandisi Joel Samwel Mwambungu, ameambatana na watumishi wote kukagua miradi mitano ya ujenzi wa madaraja ya dharura inayotekelezwa katika Wilaya za Muleba na Bukoba, kufuatia athari za mvua kubwa za El Niño zilizonyesha mwaka 2024.

Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa daraja la Kanono ambalo limekamilika kwa asilimia 100, Kyanyabasa asilimia 77, Kamishango asilimia 98, Kyetema asilimia 77, pamoja na daraja la Karebe lililofikia asilimia 73 ya utekelezaji.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mhandisi Mwambungu alisema ameridhishwa na kasi pamoja na ubora wa utekelezaji wa miradi hiyo, huku akiwaagiza wakandarasi kuhakikisha kuwa miradi yote inakamilika ifikapo Februari 20 mwaka huu kama ilivyopangwa.

Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi hiyo kwa lengo la kuwaondolea wananchi changamoto ya kukatika kwa mawasiliano ya barabara, hasa wakati wa msimu wa mvua, ambapo baadhi ya maeneo yamekuwa yakikumbwa na tatizo la barabara kutopitika kwa miaka mingi na kuleta changamoto.

Kukamilika kwa ujenzi wa madaraja hayo kutachangia kwa kiasi kikubwa kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi, kuboresha usafirishaji wa mazao na huduma mbalimbali, pamoja na kuharakisha maendeleo ya wananchi wa maeneo husika na kuwaunganisha na mikoa mingine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *