ZANZIBAR: WAANDAAJI wa Tamasha la Sauti za Busara toleo la 23 wamesema tamasha hilo litafanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Unguja, badala ya Ngome Kongwe kuanzia Februari 5 hadi 8 mwaka huu.
Uamuzi huo umetokana na ongezeko kubwa la idadi ya watazamaji kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na kazi za ukarabati zinazoendelea katika Ngome Kongwe.
Hali iliwalazimu waandaaji kutafuta eneo lenye uwezo mpana zaidi wa kuhudumia mahitaji ya tamasha hilo maarufu kimataifa.
Ilielezwa kuwa eneo jipya la Mnazi Mmoja litatoa nafasi kubwa zaidi kwa wasanii na wadau, likiwa na majukwaa mawili ya maonesho, soko la bidhaa za ndani, maeneo ya chakula, kivuli cha miti ya kihistoria pamoja na urahisi wa upatikanaji wa usafiri wa umma na watembea kwa miguu.
Akizungumzia maandalizi hayo, Mkurugenzi wa Tamasha, Journey Ramadhan alisema tamasha la mwaka huu limepokelewa vyema na wapenzi wa muziki hivyo linatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Alisema ujio wa gwiji wa muziki wa Afrika, Salif Keita kutoka Mali umeongeza kwa kiasi kikubwa hamasa ya mashabiki, mahitaji ya tiketi pamoja na nafasi za malazi visiwani Zanzibar.
Ramadhan aliongeza kuwa waandaaji wamefanya kazi kwa karibu na Serikali kuhakikisha tamasha linafanyika kwa usalama, mpangilio mzuri na kwa viwango vya kimataifa.
Tamasha la Sauti za Busara 2026 linatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya wanamuziki 400 kutoka nchi 21 likiwa jukwaa la kuenzi umoja na mshikamano kupitia muziki, sambamba na kuendeleza programu za kijamii za kuwawezesha wanawake katika tasnia ya muziki.