Roma, Italia. Staa straika Mario Balotelli sasa amekamilisha mpango wake wa kujiunga na klabu ya 14 katika maisha yake ya soka baada ya kuibuka upya kwa kujiunga na Al-Ittifaq ya Dubai.
Fowadi huyo Mtaliano aliyetumikia nusu ya kwanza ya msimu huu akiwa mchezaji huru baada ya kuondoka Genoa wakati mkataba wake ulipofika tamati Juni mwaka jana. Balotelli amezivutia timu nyingi za Major League Soccer na Liga MX kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi, lakini alishindwa kupata timu ya kujiunga nayo. Staa huyo mwenye umri wa miaka 35, alitunza kiwango chake wakati alipokuwa akicheza na kuwa kocha huko Kandima, Maldives, na sasa amepata kabisa timu ya kuitumikia huko Falme za Kiarabu.
Balotelli amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu huko Al-Ittifaq. Hii sio ile timu ya Saudia aliyoinoa Steven Gerrard. Badala yake, klabu hiyo ya Falme za Kiarabu, ilianzishwa miaka sita iliyopita na sasa inashika mkia kwenye ligi ya UAE First Division.
Al-Ittifaq imeshinda mechi mbili tu kati ya 11 ilizocheza msimu huu, huku ikiwa imefunga mabao sita, hivyo inamhitaji Balotelli kuja kuokoa jahazi.
Hata hivyo, straika huyo ambaye zama zake kwenye soka la Ulaya zinaonekana kumpa kisogo, alishindwa kufunga bao lolote katika mechi sita alizochezea Genoa msimu uliopita. Na sasa timu hiyo inakuwa klabu ya 14 katika maisha ya Balotelli, tangu kuanzia uhamisho wa kujiunga na Inter Milan mwaka 2007 wakati huo alipokuwa kinda akitokea Lumezzane.
Alikuwa sehemu ya kikosi cha Nerazzurri kilichotwaa mataji matatu makubwa ndani ya msimu mmoja chini ya kocha Jose Mourinho, likiwamo taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2010. Asisti yake maarufu kwenye Ligi Kuu England ni ile ya bao la Sergio Aguero, ambalo liliifanya Manchester City kunyakua taji hilo mwaka 2012. Baada ya kutibuana na kocha wa Man City, Roberto Mancini, Balotelli aliondoka na kwenda AC Milan.
Baadaye, Super Mario alirudi Ligi Kuu England, safari hi akijiunga na Liverpool katika majira ya kiangazi 2014. Kisha aliondoka kwenye kujiunga na Nice ya Ufaransa baada ya mkopo AC Milan. Tangu wakati huo, Balotelli hajawahi kudumu kwenye timu moja kwa zaidi ya msimu mmoja, akipita Ligue 1, Serie A, Uswisi na Uturuki. Balotelli amefunguka pia kwa sasa anafikiria kuwa kocha akiamini kwa umri wake anapaswa kuwapisha wengine.
KLABU ALIZOPITA BALOTELLI HIZI HAPA
2006 – Lumezzane
2007–2010 – Inter Milan
2010–2013 Man City
2013–2014 AC Milan
2014–2016 Liverpool
2015–2016 → AC Milan (mkopo)
2016–2019 Nice
2019 Marseille
2019–2020 Brescia
2020–2021 Monza
2021–2022 Adana Demirspor
2022–2023 Sion
2023–2024 Adana Demirspor
2024–2025 Genoa
2026– Al-Ittifaq