
Serikali ya Uganda imeamuru mashirika mawili ya ndani ya kutetea haki za binadamu kusitisha shughuli zao, zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu ambao Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu imeutaja kuwa unafanyika katika mazingira ya ukandamizaji na vitisho.
Mashirika yaliyoathiriwa ni Chapter Four Uganda na Human Rights Network for Journalists–Uganda, HRNJ-U. Mashirika hayo yamelaani hatua hiyo, na kusema uamuzi huo ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Pia yametoa madai ya kukamatwa kiholela na kuteswa kwa wafuasi wa upinzani pamoja na wanahabari.
Katika barua kwa Chapter Four na iliyooonekana na shirika la habari la Reuters, Ofisi ya Kitaifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali inayosimamiwa na serikali ya Uganda, imedai kuwa shirika hilo linajihusisha na shughuli “zinazohatarisha” usalama wa taifa, na hivyo limetakiwa kusitisha kazi zake mara moja.
Rais Yoweri Museveni aliyeingia madarakani mwaka 1986 baada ya uasi wa miaka mitano, ni miongoni mwa viongozi waliodumu madarakani kwa muda mrefu barani Afrika.
Ameshabadilisha katiba mara mbili ili kuondoa kikomo cha umri na cha mihula ya urais, na ushawishi wake mkubwa ndani ya taasisi za serikali unaashiria uwezekano mdogo wa kushindwa katika uchaguzi wa Januari 15.
