Helsinki. Tanzania imeshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Matka yanayofanyika jijini Helsinki, Finland, kuanzia Januari 14 hadi 18, 2026, ambayo yameratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden.

Katika maonesho hayo, Tanzania imetangaza vivutio vyake vya utalii pamoja na kuonesha filamu ya Tanzania: The Royal Tour, inayolenga kuitangaza nchi kimataifa zaidi.

Matka ni miongoni mwa maonesho makubwa barani Ulaya, yakishirikisha zaidi ya kampuni 950 za utalii, mashirika ya ndege, vyombo vya habari na taasisi za ushauri wa utalii kutoka mataifa mbalimbali.

Aidha, siku ya kwanza pekee, maonesho hayo yalipokea zaidi ya washiriki 56,000, wakiwemo watalii watarajiwa.

Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi, akizungumza na Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni ya GapEdu ya Finland, Jyrki Nilson, kwenye banda la Tanzania wakati wa Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Matka, yanayoendelea jijini Helsinki, Finland.

Kampuni binafsi za Kitanzania za Lifestyle Safaris & Holidays na Lifetime Safaris nazo zilishiriki maonesho hayo kwa kushirikiana na timu ya Ubalozi wa Tanzania. Mbali na Tanzania, nchi nyingine za Afrika zinazoshiriki ni Uganda, Kenya, Ushelisheli, Namibia, Afrika Kusini, Senegal, Morocco, Tunisia na Misri.

Akizungumza katika maonesho hayo, Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi, ambaye pia anaiwakilisha Tanzania katika nchi za Nordic, Baltic na Ukraine, amesema Tanzania imeendelea kupata heshima kimataifa baada ya kushinda Tuzo za Utalii za Dunia (World Travel Awards) Desemba 9, 2025 nchini Bahrain, ikiwa ni mwaka wa tatu mfululizo.

Balozi Matinyi pia ameeleza kuhusu ushiriki wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika filamu ya Tanzania ya The Royal Tour, iliyorekodiwa mwaka 2022 kwa kushirikiana na mwandishi wa habari wa Marekani na mshindi wa Tuzo ya Emmy, Peter Greenberg.

Amebainisha kuwa Tanzania ina vivutio vitatu kati ya Maajabu Saba ya Asili ya Afrika, pamoja na maeneo saba yaliyotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kama Urithi wa Dunia.

Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi (kulia) pamoja na Ofisa Ubalozi, Abel Maganya, wakizungumza na Peter Hallgren wa kampuni ya Flygresor ya Sweden kwenye banda la Tanzania wakati wa maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Matka, yanayoendelea jijini Helsinki, Finland.

Vivutio hivyo ni pamoja na Mlima Kilimanjaro, hifadhi ya Serengeti yenye uhamaji mkubwa wa wanyamapori, na Bonde la Ngorongoro.

Vilevile Tanzania ina hifadhi za taifa 22, makabila zaidi ya 126 yenye utamaduni wa kipekee, pamoja na maeneo ya kihistoria kama michoro ya mapangoni ya Kondoa, Mji Mkongwe wa Zanzibar, Bagamoyo na Kilwa.

Katika maonesho hayo, Balozi Matinyi pia amefanya mazungumzo na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii kutoka Ulaya, akiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Atlantic Link ya Denmark, Karin Gert Nielsen; mwakilishi wa Danish Travel Show, Johnny Frandsen; na Meneja wa Flygresor ya Sweden, Peter Hallgren.

Wengine aliokutana nao ni Mwanzilishi na Mkurugenzi Mwendeshaji wa GapEdu, Jyrki Nilson; Mkurugenzi Mwendeshaji wa Amanihoiva Limited, Juha Valtanen; na Mwakilishi wa Matka Travel Fair, Inkeri Vainik, wote kutoka Finland.

Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kuitangaza zaidi Tanzania kama kitovu cha utalii barani Ulaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *