
Mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa kaskazini-mashariki mwa Afrika Kusini yamesababisha vifo vya watu 10 kwa usiku mmoja na kupelekea kufungwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kruger.
Idara ya Hali ya Hewa ya Afrika Kusini imetahadharisha kuwa mvua kubwa zinatarajiwa kunyesha katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo huku nchi jirani Msumbiji pia ikiwa katiak hali ya tahadhari baada ya mafuriko kubomoa nyumba na barabara.
Watu tisa wamepoteza maisha katika kijiji kimoja katika jimbo la Limpopo nchini Afrika Kusini karibu na HIfadhi ya Taifa ya Wanyamapori ya Kruger. Wakati huo huo hadi sasa watu karibu 200 wamehamishwa katika maeneo salama.
Picha zilizotolewa na jeshi la ulinzi la Afrika Kusini zimeonyesha helikopta ya jeshi ikiwahamisha watu kadhaa waliokuwa wamekwama katika miji kufuatia mafuriko makubwa yaliyoiathiri nchi hiyo. Katika jimbo la Mpumalanga wafanyakazi wa huduma za uokoaji jana waliupata mwili wa mwanamke aliyefariki dunia ambaye alizama wakati akijaribu kuvuka mto.
Takriban watu 19 wamekufa huko Mpumalanga tangu mvua ianze kunyesha mwezi Novemba, amesema msemaji wa jimbo hilo Freddy Ngobe aliozungumza na shirika la habari la AFP.
Jana Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini alitembelea jimbo la Limpopo “ili kutathmini ukubwa wa uharibifu na maafa na hatua zinazopaswa kuchukuliwa na serikali.