Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO kanda ya Afrika kupitia taarifa yake iliyotolewa leo huko Nairobi, Kenya linasema ukame wa muda mrefu umesababisha ongezeko la utapiamlo, hatari ya milipuko ya magonjwa, na kuvurugika kwa huduma muhimu za afya.

Mvua za mwaka 2025 zilinyesha kwa asilimia 30 hadi 60 tu ya wastani wa kawaida, jambo lililoufanya kuwa msimu mkavu zaidi tangu mwaka 1981 katika baadhi ya maeneo ya mashariki mwa Kenya.

Athari hizo mbaya pia zimeripotiwa katika nchi jirani za Tanzania, Uganda, na Somalia, ambapo mamilioni ya watu wako hatarini kutokana na uhaba wa maji na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kaunti zilizoathirika vibaya nchini Kenya

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Ukame nchini Kenya, kaunti 10 ziko katika hali mbaya. Kaunti tisa – zikiwemo Wajir, Garissa, Kilifi, Marsabit, Kitui, Kwale, Kajiado, Isiolo, na Tana River ziko katika hatua ya “tahadhari”, huku kaunti ya Mandera ikiwa katika hatua ya hatari zaidi.

Kaunti nyingine 13 katika maeneo ya Kavu na yale yenye Ukame, (ASAL) ambazo kwa sasa bado zimeorodheshwa kuwa katika hali ya “kawaida,” zimeanza kuonesha dalili za wazi za kudhurika na ukame.

 Dalili hizi zinaonekana zaidi kutokana na kupungua kwa kina cha maji kwenye visima na mabwawa pamoja na mifugo kudhoofika kutokana na ukosefu wa malisho na maji.

Serikali ya Kenya imeonya kuwa idadi hiyo inaweza kufikia watu milioni 2.5 ikiwa ukame utaendelea.

Dkt. Martins, Mkuu wa Idara ya WHO nchini Kenya ya Kujiandaa na Kukabiliana na Dharura, ameeleza kuwa uhaba wa maji unawalazimu watu kutumia vyanzo visivyo salama:

“Tunaona vitisho vingi vya kiafya vikikutana. Uhaba wa maji unalazimu familia kutegemea vyanzo visivyo salama, jambo linaloongeza hatari ya kipindupindu, homa ya matumbo, na magonjwa ya kuhara. Aidha, mifugo inayotegemewa kwa chakula imeathirika, na kuwaacha watoto na wanawake wajawazito katika hatari kubwa ya utapiamlo.”

Dkt. Martins ameongeza kuwa ukame huu umekausha ardhi kiasi kwamba mvua ikinyesha, kuna hatari kubwa ya mafuriko ya ghafla ambayo yataleta magonjwa zaidi ya mlipuko.

Katika harakati za kujiandaa, mnamo Novemba 2025, WHO ilikabidhi vifaa vya dharura kwa serikali ya Kenya, vikiwemo vifaa vya kutibu kipindupindu, vichomi au numonia, na mahitaji mengine muhimu katika kaunti zenye hatari kubwa. Hata hivyo, msaada zaidi unahitajika ili kukidhi ukubwa wa janga hili.

Wito wa WHO Kenya

Dkt. Neema, Kaimu Mwakilishi wa WHO nchini Kenya, ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka:

“Kipaumbele chetu cha sasa lazima kiwe kuhakikisha jamii zinapata chakula cha kutosha na maji salama kwa binadamu na mifugo. Juhudi za pamoja zinahitajika ili kuzuia hali isiwe mbaya zaidi.”

Ili kuhakikisha hatua zinazochukuliwa zinategemea ushahidi wa kisayansi, WHO imesaidia Wizara ya Afya ya Kenya na Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Jamii (NPHI) kupanga ramani ya vihatarishi vya afya vya kila mwaka.

Kazi hii imefanyika kwa kutumia kifaa cha kimkakati cha kutathmini vihatarishi kinachojulikana kama STAR (Strategic Tool for Assessing Risks).

Hii ni seti ya zana za kisasa za WHO zinazotumika kufanya tathmini ya kina ya vihatarishi vya afya ya jamii kwa kuzingatia ushahidi, jambo linalosaidia mamlaka kutabiri majanga, kubaini maeneo yenye hatari kubwa ya ukame au milipuko ya magonjwa kabla hayajatokea, kupanga rasilimali na kupeleka dawa na vifaa kwenye kaunti zenye hatari zaidi kabla hali haijawa mbaya.

Kwa sasa, jamii nchini Kenya zinasubiri kwa hamu msimu wa mvua ndefu za Machi-Aprili-Mei, huku mashirika ya kibinadamu yakihimiza uimarishaji wa huduma za afya, lishe, na maji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *