Miaka minne tangu ilipojiondoa Marekani, kwa mara nyingine tena Afghanistan imegeuzwa nukta kuu inayoangaziwa na madola yenye nguvu duniani.

Hata hivyo mara hii si kwa utumiaji silaha. Kutokana na akiba kubwa iliyonayo ya madini yenye thamani ya mabilioni ya dola pamoja na kuwa kwake katika eneo la kimkakati, Afghanistan imekuwa uwanja wa “shindano jipya kubwa” ambalo limezikutanisha China, Russia na India kwenye mpambano mkali.

Afghanistan inapitia kwenye mabadiliko ya kihistoria kutoka kwenye hali ya “tatizo la kiusalama” hadi kuwa “fursa ya kimkakati”. Akiba yake kubwa ya madini ya lithiamu na shaba, pamoja na kuwepo Afghanistan kwenye eneo la njia ya kipekee ya upitishaji bidhaa, vimeifungulia njia nchi hiyo ya kurejea kwenye ramani ya kimataifa ya kijiopolitiki.

China imekuwa ya mbele kufuatilia matarajio yake ya kiuchumi kwa kuongoza katika kumpokea balozi wa Taliban na kuialika Kabul ijiunge na “Mpango wa Ukanda na Barabara”. Russia inapigania kuimarisha satua na ushawishi wake katika Asia ya Kati kwa kuiondoa Taliban kwenye orodha ya magaidi na kuitaja kama “mshirika katika mapambano dhidi ya ugaidi.”

India nayo, licha ya kutoitambua rasmi Taliban, imechukua hatua za kivitendo za kujitosa kwenye ulingo wa milingano mipya kwa kufungua ofisi yake ya uwakilishi mjini Kabul na kumpokea balozi wa kundi hilo. Mvutano uliopo kati ya Taliban na Pakistan umefungua dirisha la fursa kwa New Delhi.

Nazo nchi za Asia ya Kati, ambazo zimeshatambua hali halisi mpya iliyojitokeza, zimechukua hatua kuanzia kuiondoa Taliban kwenye orodha ya magaidi hadi kuanzisha nayo uhusiano wa kidiplomasia ili kuweza kunufaika na njia ya kipekee ya Afghanistan ya upitishaji bidhaa.

Hata hivyo mgongano uliopo katika mabadiliko yote haya ni kuanzishwa makundi ya mawasiliano ya kikanda, ambayo kwa upande mmoja, yanatoa miito ya kuwepo utulivu na uthabiti nchini Afghanistan, lakini kwa upande mwingine, yanafuatilia mienendo ya Taliban. Ijapokuwa mchakato huu unaambatana na changamoto za kiusalama, lakini unaonyesha kuwa Afghanistan haiwezi tena kupuuzwa. Mustakabali wa Afghanistan hautaamuliwa kwenye medani za vita, lakini kwenye meza za mazungumzo ya kiuchumi na kimkakati ya kikanda.

Afghanistan iliyo chini ya utawala wa Taliban imegeuzwa kuwa kitovu cha mazungumzo ya pande kadhaa za kikanda. Kuanzishwa “Kundi la Mawasiliano la Asia ya Kati” linalojumuisha nchi za Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan na Uzbekistan, pamoja na “Kundi la Pande Nne” linalojumuisha Iran, Russia, China na Pakistan, kunaonyesha uelewa wa pamoja uliopo katika eneo hili juu ya ukweli kwamba utulivu na uthabiti wa Afghanistan ni sharti la lazima kwa ajili ya usalama na maendeleo ya nchi zote jirani.

Mawaziri wa “Kundi la Pande Nne” linalojumuisha Iran, Russia, China na Pakistan

Nukta muhimu na ya kuzingatiwa hapa ni kwamba, mustakabali wa Afghanistan hauamuliwi tena katika mji wa Kabul tu. Miji mikuu ya eneo, kuanzia Moscow hadi Beijing na kutoka Tehran hadi Tashkent yote ina nafasi za kuchangia katika kutoa muelekeo wa mabadiliko yanayojiri nchini humo. Japokuwa ushirikiano huo wa pamoja umejaa changamoto, lakini unaweza kufungua njia ya kuitoa Afghanistan kweli hali ya kutengwa na kuiunganishwa taratibu kwenye milingano ya kikanda…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *