Madrid, Hispania. Mabosi wa Real Madrid wamewasiliana na kambi ya Erling Haaland ili kuangalia uwezekano wa kumsajili, huku ripoti zikidai kabla ya kufanikisha hilo wanataka kwanza kumuuza staa wao wa kimataifa wa Brazil, Vinicius Jr.
Ripoti kutoka tovuti ya Daily Briefing zinaeleza Madrid inaweza kuwa na fedha nyingi za kutumia dirisha lijalo la majira ya kiangazi ikiwa itafanikisha mchakato wa kumuuza Vinicius Junior kwenda Saudi Arabia ambako kuna timu ipo tayari kutoa ada ya uhamisho ya takribani Euro 250 milioni.
Hata hivyo, kwa sasa, Man City imeweka wazi haitaki kumuuza Haaland na mchezaji mwenyewe inadaiwa hana nia ya kuondoka kwenye viunga vya Etihad Stadium.
Licha ya kutohitaji kumuuza, inaelezwa Madrid haijakata tamaa na inaamini ikiwa itawasilisha ofa nono kuna uwezekano timu hiyo ikabadili mawazo.
Man City haina presha yoyote ya kumuuza Haaland kwani mchezaji huyo wa miaka 25 alisaini mkataba mpya hivi karibuni ambao utadumu hadi mwaka 2034.
Mpango wa Madrid ni kuongeza nguvu zaidi katika eneo lao la ushambuliaji kwani wanaamini Haaland akiungana na Mbappe wanaweza kutengeneza safu hatari zaidi.
Madrid pia inasikilizia matokeo ya mashtaka zaidi ya 100 ambayo Man City yanawakabili na inaamini ikiwa timu hiyo itapigwa faini au kukatwa pointi inaweza kuwa sababu moja wapo ya wao kumpata Haaland kwani moja kati ya adhabu zinazoweza kutolewa ni pamoja na matajiri hao wa Jiji la Manchester kushushwa daraja.
Vinicius anayetajwa atauzwa mwisho wa msimu huu ili kupata pesa za kumnunua Haaland, tangu kuanza kwa msimu huu anadaiwa kuwa hana furaha na kinachoendelea katika timu na mara kadhaa amekuwa akiwekwa benchi na kocha mpya Xabi Alonso.