Matarajio ni kwamba mataifa yatawasilisha michango mipya ya kitaifa (NDCs) pamoja na kuendeleza ahadi zilizotolewa wakati wa COP29 mwaka uliopita. Mkutano huo pia unatarajiwa kutafuta mbinu bunifu za ufadhili ili kusaidia nchi zinazoathirika zaidi na janga la tabianchi.

Katika hafla ya ufunguzi, Simon Stiell ambaye ni Katibu Mtendaji wa UNFCCC amesema matarajio ya miaka 10 iliyopita huko Paris ya kupunguza utoaji wa hewa chafuzi si haba yanaonekana lakini bado kuna changamoto ya kuhakikisha ongezeko la joto halivuki kiwango cha nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi.

Huu si wakati wa kulalamika bali kuchukua hatua

Hata hivyo amesema huu si wakati wa kulalamika  bali ni wakati wa kusaka majawabu. “Tumekuja hapa Belém kwenye mdomo wa mto Amazon. Na tunaweza kujifunza mengi kutoka mto huu mkuu. Amazon si kitu kimoja pekee, bali ni mfumo mkubwa wa mito unaoungwa mkono na zaidi ya vijito 1,000. Ili kuharakisha utekelezaji, mchakato wa COP lazima uungwe mkono kwa njia hiyo – ukiendeshwa na mikondo mingi ya ushirikiano wa kimataifa –kwa sababu ahadi za kitaifa pekee hazipunguzi utoaji wa hewa chafuzi kwa kasi ya kutosha.”

Changamoto ni kubwa, chaguo li wazi – Guterres

Awali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X amesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua kwa haraka na kwa pamoja akiandika, “Umoja wa Mataifa hautakubali kushindwa katika lengo la nyuzijoto 1.5. Changamoto ni kubwa, lakini chaguo ni wazi. Tunahitaji kusonga kwa kasi zaidi  na kwa umoja. Tuchochee muongo wa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kutekeleza ahadi zetu.”

Kila taifa lina haki ya kulinda haki ya binadamu kwenye mazingira

Naye Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, amesisitiza kwamba COP30 inapaswa kuwa “mgeuko muhimu” katika kuhakikisha uwajibikaji wa mataifa kuhusu tabianchi na haki za binadamu.

Türk amesema, “Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imeweka wazi kwamba kila taifa lina wajibu wa kulinda haki za binadamu mbele ya mabadiliko ya tabianchi. Ukubwa na dharura ya janga hili vinahitaji hatua za mageuzi zinazojikita katika haki za binadamu.”

Wakimbizi wa madhara ya mabadiliko ya tabianchi waongezeka

Nayo mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa yameangazia zaidi upande wa kibinadamu wa tatizo hili. Ripoti mpya ya UNHCR imeonesha kwamba matukio makali ya hali ya hewa yanasababisha watu kuhama mara kwa mara, hasa katika maeneo yenye migogoro, huku Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) likitumia jukwaa la COP30 kusisitiza umuhimu wa kuweka binadamu katikati ya hatua za kukabiliana na tabianchi.

Mkutano huo wa wiki mbili mjini Belém ukiwa wa kwanza kuandaliwa na Brazil baada ya zaidi ya muongo mmoja unalenga kuimarisha juhudi za dunia kuelekea ustahimilivu wa tabianchi, usawa na maendeleo endelevu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *