Wakati mji wa Goma ukijaribu kurejea katika hali ya utulivu, vita nyingine inaendelea kimyakimya, vita ya ukatili wa kingono. Katika vitongoji vya pembezoni mwa jiji, ambako usalama bado sio wa uhakika, wanawake wengi wanaendelea kupitia mateso ya ukatili wa hali ya juu, ikiwemo kubakwa na hata kukeketwa sehemu za siri. Ukatili huu, unaofanywa mara nyingi usiku na watu wenye silaha, umeacha nyuma yake majeraha ya miili na nafsi zilizovunjika.

Daktari Aimé Manga amejipa jukumu la kurekebisha yale ambayo vita imeharibu. Ni daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika hospitali ya Rehema mjini Goma, anayewatibu bure waathirika wa  ukatili wa kingono na wanawake waliokeketwa.

Katika Hospitali ya Rehema, Dokta Aimé Manga huwapokea wanawake waliobakwa na walioumizwa. Yeye ameamua kujitolea kikamilifu kurejesha afya ya miili na nafsi zao, bila malipo, bila ufadhili, na yote hayo kwa moyo wa kibinadamu tu.

“Hata sisi madaktari, kwa namna fulani, tumepata mshtuko wa kisaikolojia. Lakini tufanye nini? Tunapokuwa tukiwatibu hawa wanawake, tunafanya kwa umakini mkubwa kwa sababu tunajiambia, ni sasa au kamwe, ” alisema Daktari Manga.

Vitendo vya ubakaji vyaongezeka mashariki mwa DRC

Goma | Dr. Aimé Manga na timu yake wakiwa katika chumba cha upasuaji
Dr Aimé Manga akiwa na timu yake tayari kwa upasuaji wa mwanamke aliyebakwa huko Mashariki mwa DRCPicha: Ruth Alonga/DW

Tangu mwanzo wa vita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, visa vya ubakaji vimeongezeka kwa kiwango cha kutisha, mara nyingi vikifanywa kama silaha ya kivita. Lakini, kwa mujibu wa wahudumu wa afya, sasa kuna aina mpya ya ukatili: ukeketaji kwa wanawake kama alivyoeleza Prince Amani, ambaye ni mwanasaikolojia akisema kuwa kesi za ukeketaji zinatofautiana kati ya wanawake 15 hadi 20 kila mwezi.

Kwa wastani,  zaidi ya wanawake 20 waliokeketwa au kubakwa  hutibiwa kila mwezi katika Hospitali ya Rehema. Baada ya upasuaji, wanapata ushauri wa kisaikolojia, hatua ya kwanza kuelekea uponyaji wa kweli.

Tangu kusimamishwa kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani, USAID, upatikanaji wa vifaa muhimu kama vile dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (PREP), umekuwa mgumu sana. Dawa hizo ndizo zinazotumika kuzuia maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI, mimba zisizotarajiwa, na maambukizi mengine kwa waathirika wa ubakaji. Daktari Aimé amesema sasa wanalazimika kutumia mbinu mbadala.

”Mwanamke anapobakwa, ni muhimu kumpatia PREP ili kuzuia mimba au maambukizi kama vile VVU. Kwa sasa, kwa kuwa hatuna dawa za PREP, tunatumia dawa za ARV kuzuia maambukizi ya VVU. Pia tunatoa antibiotiki kwa ajili ya kuzuia maambukizi mengine, na dawa za kuzuia mimba zisizotarajiwa,” alieleza daktari huyo.

Harakati hizo zakabiliwa na vikwazo mbalimbali

Bila ufadhili wa kudumu, kutokana na kupungua kwa shughuli za mashirika ya kibinadamu kufuatia kusitishwa kwa msaada wa USAID, na kufungwa kwa uwanja wa ndege wa Goma, usambazaji wa dawa umekuwa changamoto kubwa. Hata hivyo, kila siku daktari Aimé Manga anaendelea na kazi yake ya kuokoa maisha huko  mashariki mwa DRC.

Ndani ya chumba cha upasuaji, mikono yake inafanya kazi kwa utulivu na umakini. Kila upasuaji ni jaribio la kurejesha heshima. Leo, mgonjwa mpya kijana wa kike aliyekeketwa, yuko chumba cha upasuaji. Mfano msichana mmoja aliyefanyiwa upasuaji kwa zaidi ya saa moja kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa fistula.

”Tulichukua zaidi ya saa moja. Saa moja ni muda mrefu, lakini kwa mwanamke hupaswi kuwa na haraka. Inabidi kufanya kila kitu taratibu kutoka mwanzo hadi mwisho, ” alieleza Dkt. Aimé Manga.

DRC | Wanawake wa Mashariki mwa Kongo wamekuwa wakifanyiwa ukatili mkubwa
Wanawake, watoto na raia wengine wa Mashariki mwa Kongo wakijaribu kupata msaada Picha: ALEXIS HUGUET/AFP

Amina, mwenye umri wa miaka 18, alibakwa na wanaume watano wenye silaha alipokuwa akitoka sokoni. Kumbukumbu hiyo mbaya haimtoki kamwe.

”Nilikiona kifo usoni. Ndani ya nyumba kulikuwa na wavulana wawili, waliwapiga kwa nyundo. Tukio hili linaniumiza moyo, na ninapolia, naishiwa nguvu, ” alisema mwanamke huyo.

Kwa upande wake, Beatrice, mwenye umri wa miaka 32, aliyefanyiwa upasuaji wiki moja iliyopita, sasa anaweza kutabasamu tena: ” Kwa sababu ya Daktari Aimé, nimepata tena imani. Najua siku moja nitatembea kama zamani. Hakuna maumivu yatakayoweza kunishinda tena.”

Huko  Goma , nyuma ya takwimu na ripoti, kuna nyuso halisi, miili iliyo na majeraha, lakini pia wanawake wanaosimama tena. Wanawake wanaokataa kufungwa katika maumivu waliyopitia. Na kuna watu kama Dkt. Aimé Manga, wanaoendelea kila siku bila kuchoka na bila ya kuwa na msaada mkubwa, kusikiliza, kutibu na kuyajenga upya maisha ya wanawake hao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *