Dar es Salaam. Licha ya kipindi kigumu anachopitia akiwa na kikosi cha Yanga msimu huu, mshambuliaji Prince Dube ameendelea kuwa muhimu katika timu ya Taifa ya Zimbabwe baada ya kuitwa katika kikosi cha wachezaji 24 kwa ajili ya mechi mbili za kimataifa za kirafiki zitakazochezwa baadaye mwezi huu.

Dube ambaye ni miongoni mwa nyota 24 wa Zimbabwe walioitwa na Kocha Mario Marinica, hadi sasa hajaifungia Yanga bao katika mechi nne ambazo timu hiyo imecheza katia Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Pamba Jiji, Mbeya City, Mtibwa Sugar na KMC.

Zimbabwe itacheza na Algeria Novemba 13 jijini Jeddah, Saudi Arabia, kisha kumenyana na Qatar siku nne baadaye.

Washington Navaya mwenye umri wa miaka 27 ndiye mchezaji pekee mpya kwenye kikosi hicho akiitwa kipindi hiki anapoelekea kumaliza akiwa Mfungaji Bora wa ligi ya Zimbabwe msimu huu. 

Tymon Machope anarejea kikosini, sawa na kiungo wa kati Sean Fusire mwenye umri wa miaka 20, anayechezea Sheffield Wednesday.

Prosper Padera anayecheza soka la kulipwa Finland pia amerejea, baada ya mwezi uliopita kusherehekea siku yake ya kuzaliwa ya 20, na kuchukua nafasi ya kiungo wa Wolverhampton Wanderers Marshall Munetsi.

Khama Billiat anayecheza Scotand ni mchezaji mwingine mashuhuri ambaye hayupo kwenye kikosi.

Kikosi cha Zimbabwe kinaundwa na makipa Washington Arubi (Marumo Gallants), Elvis Chipezeze (Magesi) na  Martin Mapisa (Moors World of Sport) huku mabeki wakiwa ni Munashe Garananga (FC Copenhagen), Brandon Galloway (Plymouth Argyle), Teenage Hadebe (FC Cincinnati), Emmanuel Jalai (Dynamos), Divine Lunga (Mamelodi Sundowns), Godknows Murwira (Scotland FC) na Gerald Takwara (Al Ittihad Misurata).

Viungo ni Tawanda Chirewa (Wolverhampton Wanderers), Jonah Fabisch (Erzgebirg Aue), Sean Fusire (Sheffield Wednesday), Daniel Msendami (Marumo Gallants), Marvelous Nakamba (Luton Town), Prosper Padera (Seinäjoen Jalkapallokerho) na Jordan Zemura (Udinese).

Kikosi hicho kina washambuliaji Bill Antonio (KV Mechelen), Prince Dube (Yanga), Tymon Machope (Scotland FC), Tawanda Maswanhise (Motherwell), Knowledge Musona na Walter Musona (Scotland fc) pamoja na Washington Navaya (TelOne).

Mechi hizo mbili ni za maandalizi ya mwisho kwa ajili ya Fainali za AFCON 2025 zitakazofanyika Morocco kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026.

Katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, Zimbabwe imepangwa katika Kundi B ikiwa na timu za Misri, Afrika Kusini na Angola.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *